Wednesday, 22 June 2016

LUKUVI ATOA SIKU KUMI UTATUZI WA MGOGORO WA MAKAZI MAGOMENI


Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Willium Lukuvi ametoa siku 10 kwa watendaji wa wizara yake kumshauri aweze kutatua mgogoro wa makazi wa watu wa Kinondoni Quarters, jijini Dar es Salaam.

Akisikiliza malalamiko ya wakazi hao leo, Lukuvi alisema kazi ya serikali kwa sasa ni kuona haki za wananchi zinapatikana kwa muda muafaka na kuondoa ubabaishaji usiokuwa na tija.

“Kazi ya serikali ya awamu ya tano ni kurekebisha yaliyopinda na kutoa suluhu haraka ili kuwafuta wananchi machozi,” alisema Lukuvi.

Aliongeza kuwa nia ya serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapatiwa makazi bora na kwa sasa wizara inafanya mapitio ya Sera ya Makazi ya mwaka 2010 ili iweze kwenda na wakati na pia kutengeneza sera ya nyumba.

Awali akitoa malalamiko hayo, mwenyekiti wa kamati ya wakazi waliovunjiwa nyumba zao, George Abel alisema kuwa suala hilo limechukua muda mrefu tangu mwaka 2009 hivyo kumuomba waziri amshauri Rais John Magufuli abatilishe umiliki wa ardhi hiyo na kuukabidhi kwa wizara ya ardhi ili nyumba zijengwe upya.

Abel alisema kuwa wakazi 644 wa Kinondoni quarters walivunjiwa nyumba zao na manispaa ya Kinondoni kwa madai kuwa ni nyumba chakavu na zitajengwa nyumba za kisasa ambazo watapangishwa na baadaye kuuziwa jambo ambalo halijatekelezwa hadi sasa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment