Thursday, 16 June 2016

KITIMOTO NA POMBE VYAHATARISHA KAYA MASIKINI KILOLO


NYAMA ya ngurume (maarufu kama kitimoto) na pombe aina ya komoni kwa pamoja zimeelezwa kuziweka kaya masikini zilizopo kijijini Itimbo wilayani Kilolo mkoani Iringa  katika hatari ya kufutwa kwenye mpango wa kunusuru kaya masikini.

Mpango huo unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) unatoa fedha kwa kaya masikini zilizotambuliwa katika maeneo mbalimbali nchini ili ziweze kuwasaidia kugharamia mahitaji yao ya msingi ikiwemo afya, elimu na lishe.

Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo alisema jumla ya kaya masikini 6,401 zikiwemo zaidi ya kaya 50 za kijiji cha Itimbo, wilayani humo zinanufaika na fedha za mpango huo ulioanza mwaka jana.

Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini haulengi tu katika kuhawilisha fedha kwa walengwa bali pia unahimiza ushiriki wa walengwa katika kazi za mikono kupitia miradi ya mbalimbali katika maeneo yao ili waweze kupata kipato, na kuwekeza" Mwaikambo alifafanua.

Kwa kupitia mpango huo, alisema kaya hizo hujipatia kati ya Sh 20,000 na Sh 70,000 kila baada ya miezi miwili, fedha zinazotolewa kulingana na vigezo mbalimbali vya umasikini kwa kila kaya.

Akizungumza na walengwa wa mpango huo kijijini Itimbo wakati malipo ya awamu ya saba yakifanywa, Mwaikambo alisema; “baadhi yenu mnazitumia fedha hizo kufanya sherehe ya unywaji pombe na uchomaji wa nyama ya nguruwe kila zinapotolewa kwa ajili ya kaya zenu.”

Huku akiwataka wabadilike, alisema wanao ushahidi unaonesha kila malipo yanapofanywa kiasi cha pombe na idadi ya nguruwe wanaochinjwa na kuuzwa huongezeka mara dufu.

Afisa ushauri na ufuatiliaji wa mpango huo wa TASAF wilayani Kilolo, Happy Mpuya alisema mpango huo ni muhimu kwa vile unatoa fursa ya ajira kwa walengwa katika kaya maskini, unawezesha kaya za walengwa kupata kipato zaidi, na unawapatia walengwa weledi na stadi za mbalimbali wakati wa utekelezaji miradi.

Mpuya alisema TASAF imeweka utaratibu wa ufuatiliaji wa matumizi ya fedha hizo hususani zinazotolewa kwa ajili ya watoto wanaotakiwa kwenda shule na wanaotakiwa kuhudhuria kliniki.

“Chakushangaza hata zile fedha zinazotolewa kwa ajili ya kuwawezesha watoto kwenda shule wakiwa katika hali nzuri na zile zinazotolewa kwa ajili ya kupeleka watoto kliniki, zote zinaliwa. Hii ni hatari kwa mpango,” Mpuya alisema.

Mpuya alisema TASAF imekwishaanza kuchukua hatua za kuwaondoa au kuwapunguzia ruzuku baadhi ya walengwa wanaozitumia fedha hizo kinyume na malengo.

Na kwa wilaya ya Kilolo, alisema wanufaika wa mpango wamepungua kutoka kaya masikini 6,464 hadi kaya 6,401, punguzo ambalo pia limeathiri kiwango cha fedha zinazopokelewa kila baada ya miezi miwili kwa ajili ya mpango huo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment