Tuesday, 19 July 2016

HUKUMU YA KESI YA MAUAJI YA DAUDI MWANGOSI YAIVAPOLISI anayetuhumiwa kuhusika na mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa Daudi Mwangosi, amekana mbele ya mahakama kuhusika na mauaji ya mwanahabari huyo aliyekuwa mwakilishi wa Channel Ten mkoani hapa akisema hamfahamu wala hakuwahi kumuona.

Baada ya kumaliza kutoa ushahidi wake uliofungwa na upande wa utetezi mwishoni mwa wiki iliyopita, Jaji anayesikiliza kesi hiyo, Paul Kiwelo alisema mahakama hiyo itatoa hukumu ya kesi ya mauaji hayo wakati wowote kuanzia sasa.

Jaji Kiwelo alisema baada ya kupokea majumuisho ya mwisho ya shauri hilo yaliyowasilishwa Ijumaa kwa njia ya maandishi kutoka upande wa utetezi na ule wa Jamuhuri, kesho (leo Jumatatu) mahakama itapokea ushauri kutoka kwa wazee wa baraza la mahakama hiyo kabla ya kupanga tarehe ya hukumu ya kesi hiyo.

Kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani hapo Septemba 12, 2012 akituhumiwa kumuua Mwangosi kwa kukusudia katika tukio lilitokea katika kijiji cha Nyololo, wilayani Mufindi Mkoani Iringa Septemba 2, 2012 wakati mwandishi huyo alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akiongozwa na wakili wake, Lwezaula Kaijage wakati akitoa utetezi wake, mtuhumiwa huyo Pacificius Cleophace Simoni (27) alikana ungamo lake alilosaini Septemba 5, 2012 kwa Mlinzi wa Amani Frola Mhelela alikiri kumuua Mwangosi na kuwajeruhi askari wengine wanne baada ya kufyatua bomu kutoka katika silaha aliyokuwa akitumia.

Alikana ungamo hilo akidai alilisaini bila kujua lina maelezo gani na yenye lengo gani kwa kupitia amri iliyotolewa na aliyekuwa Afisa Upelelezi wa Mkoa wa Iringa (RCO), Nyigesa Wankyo ambaye ni kiongozi wake kijeshi ambaye hawezi kupinga maagizo yake.

Simoni aliiambia mahakama hiyo wakati akiendelea kujitetea kwamba ungamo hilo lilipelekwa na Stafu Sajenti wa jeshi hilo aliyemtaja kwa jina moja la Erick kwa mlinzi huyo wa amani ambaye alimsainisha baada ya kulinakiri kwenye karatasi nyingine.

Alipoulizwa na wakili wa Jamuhuri, Ladslaus Komanya kama ana imani na mahakama, alisema “nina imani kubwa sana na mahakama katika utendaji wake haki.”

Alipobanwa kwanini tangu kesi hiyo ianze kusikilizwa hakumpa wakili wake taarifa hiyo ili aweze kuliwekea pingamizi ungamo hilo lililopokelewa mahakamani hapo bila pingamizi lolote kutoka kwa mlinzi huyo wa amani ambaye ni mtumishi wa mahakama hiyo alisema ni kwasababu alifungwa mdomo.

Simoni alisema anafahamu kwamba mlinzi huyo wa amani alikuwa shahidi namba tatu wa upande wa utetezi na alipotoa ushahidi kuhusiana na ungamo hilo hapakuwepo na pingamizi lolote kwasababu hiyo siyo kazi yake ni kazi ya wakili wake.

Alipotakiwa na upande wa Jamuhuri asome tena mahakamani hapo ungamo hilo alilolisaini akikiri kuhusika na mauaji ya Mwangosi alikataa kusoma akisema hajui nani aliyeandika na liliandikwa kwa lengo gani.

Baada ya Jaji kuingilia kati na kumshauri asome, mtuhumiwa huyo alisoma sehemu ya ungamo hilo akisema; “Niliondoka kutoa msaada nikiwa na long range amabyo ni silaha inayotumika kupigia mabomu ya kishindo na machozi kama inavyoonesha katika gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012.”

“Pale katika eneo la tukio bila kujua wala kufikiria likafyatua bomu, likafunguka likamuua mwandishi Daudi Mwangosi na kumjeruhi OCS ambaye alikumbatiwa na marehemu, pia kuwajeruhi askari wengine watatu waliokuwa karibu yangu na marehemu.”

Akiendelea kujitetea Simoni aliikana picha hiyo iliyotumika kumfungulia mashataka hayo ikimuonesha ameshika silaha hiyo iliyoelekezwa kwa Mwangosi kabla ya kifo hicho.

Simoni alimrushia tuhuma RCO Wankyo akisema ndiye aliyesema kwamba askari anayeonekana katika picha hiyo ni yeye kwasababu ni mwembamba kama yeye.
Mbali na Wankyo, mtuhumiwa huyo alikiri kuhojiwa kuhusiana na picha hiyo na viongozi wengine wa jeshi hilo wa wakati huo akiwemo aliyekuwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda na Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba.  

Alipoulizwa kama kulikuwa na askari wengine walikuwa na silaha kama aliyotumia yeye katika oparesheni hiyo, alisema kulikuwa na askari wengine wawili ambao hata hivyo hakuweza kuileza mahakama kama maumbile yao yanafanana na askari aliyekuwa katika picha hiyo.

Pamoja na kwamba alitumia mabomu sita (matatu ya kishindo na matatu ya machozi) kwa kupitia silaha hiyo, alisema aliirudisha katika ghala la kuhifadhia silaha mjini Iringa ikiwa katika hali nzuri; tafsiri aliyosema kwa kijeshi ina maana haikuleta madhara yoyote katika eneo la tukio.

Alipoulizwa tofauti ya silaha iliyorudishwa ikiwa katika hali nzuri na silaha iliyoleta madhara huko ilikotumika alisema anachofahamu yeye silaha ikipokelewa katika hali nzuri maana yake haikuwa na madhara huko ilikotumika.

Ilipotolewa rejista ya kutoa na kupokea silaha kama moja ya kielelezo cha kesi hiyo na alipoulizwa kama kuna mahali popote ambapo pana maelezo ya kwamba haikuwa na madhara huko ilikotumika alisema; “hiyo siyo kazi yangu ya kuandika maelezo hayo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment