Tuesday, 21 June 2016

HATMA YA MTUHUMIWA WA MAUAJI YA MWANGOSI KUFAHAMIKA KESHO


HATMA ya kesi ya mtuhumiwa wa mauaji ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Iringa (IPC), Daudi Mwangosi inasubiri uamuzi utakaotolewa kesho Jumatano (leo Juni 22) na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Paul Kiwelo baada ya upande wa Jamuhuri na ule wa utetezi jana kukamilisha kutoa ushahidi na utetezi wao.

Akitoa uamuzi huo jana baada ya maelezo ya pande hizo mbili, Jaji huyo anayesikiliza kesi hiyo alisema; “Baada ya kusikiliza shauri hili kutoka katika pande zote mbili naahirisha shauri hili mpaka kesho saa 6.00 mchana nitakapotoa uamuzi kama mshatakiwa ana kosa la kujibu au hana.”

Mwangosi aliyekuwa mwandishi wa habari wa Channel Ten aliuawa Septemba 2, 2012 katika kijiji cha Nyololo wilayani Mufindi Mkoani Iringa alipokuwa akiwajibika katika kazi zake za kutafuta habari wakati wa ufunguzi wa matawi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Kesi hiyo ambayo kila inapofikishwa mahakamani hapo imekuwa ikiwaweka wanahabari katika mazingira ya kushindwa kufanya kazi yao vizuri kutokana na vikwazo na vitisho wanavyopata kutoka kwa askari Polisi wengi wanaouhudhuria kesi hiyo, inamkabili aliyekuwa askari wa jeshi la Polisi, Pacificius Cleophace Simoni anayetuhumiwa kumuua mwandishi huyo kwa kukusudia.

Awali wakili wa upande wa utetezi Lwezaula Kaijage aliiomba mahakama hiyo imuachie huru mshatakiwa huyo kwa madai kwamba ushahidi uliotolewa na upande wa Jamuhuri umeshindwa kumtia hatiani mteja wake.

Kaijage alisema ripoti ya daktari iliyowasilishwa mahakamani hapo na upande huo wa Jamuhuri haioneshi nani aliyetenda kosa la mauaji hayo na kwamba ripoti hiyo inamuacha huru mteja wake kwasababu inaweza kutumika kumfikisha mahakamani hapo sasa au baadae mtu yoyote kuhusiana na kifo hicho cha Mwangosi.

Alisema ushahidi wa Jamuhuri umejikita katika picha ya mauaji hayo iliyochapishwa katika gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012 ambayo upande wao wa utetezi ulikataa usipokelewe mahakamani hapo kama kielelezo cha ushahidi kwasababu upande wa mashtaka ulishindwa kupeleka mahakamani hapo picha halisi iliyotumiwa na gazeti hilo na mpiga picha aliyepiga picha hiyo.

Upande wa Jamuhuri unaowakilishwa na mawakili wawili, Sandy Hyra na Ladslaus Komanya  uliiambia mahakama hiyo kwamba ushahidi uliotolewa sambamba na mashtaka yaliyowasilishwa mahakamani hapo yanaonesha mtuhumiwa huyo ana kesi ya kujibu.

“Upo ushahidi ambao hauwezi kwenda hivi hivi bila mshtakakiwa kupata fursa ya kujitetea kabla ya hukumu ya kesi hii,” alisema Wakili Komanya baada ya wakili mwenzake Hyra kutoa taarifa ya ushahidi huo.

Hyra alisema Septemba 5,2012 mshtakiwa Pacificius Cleophace Simoni alitoa ungamo kwa mlinzi wa amani na kukiri kuhusiaka na kifo hicho.

“Baadhi ya maneno katika maungamo yake, mshatakiwa alimwambia mlinzi wa amani kwamba anasikitika sana kusababisha kifo cha marehemu,” alisema wakili huyo wa Jamuhuri.

Alisema maungamo hayo yaliyotolewa mahakamani hapo kama kielelezo namba 3 cha upande wa mashtaka hayakuwa na pingamizi lolote toka kwa mshtakiwa.

Katika maungamo yake, wakili huyo alisema mshtakiwa huyo  alisema akiwa na silaha inayotumika kupigia mabomu ya kishindo na ya machozi aliungana na askari wenzake katika tukio hilo kwenda kutoa msaada kama ilivyochapishwa katika gazeti la Mwananchi la Septemba 3, 2012.

Alisema ushahidi wa shahidi wao wa kwanza unaonesha silaha hiyo ambayo matumizi yake ni lazima yafanywe na mtu inatumiwa kupiga katika digrii 40 hadi 45 na sio kwa kuelekeza kwa mtu kama alivyofanya mshatakiwa huyo.

Wakili huyo alisema aina ya kifo na majeraha aliyopata marehemu yanadhihirisha kulikuwa na kusudio la mauaji hayo na wala haikuwa bahati mbaya kwahiyo mshtakiwa ana kesi ya kujibu.

“Shahidi wetu namba moja aliileza mahakama kwamba maagizo yake kabla ya tukio hilo yalikuwa ni kuwatawanya waandamanaji. Mwangosi aliuawa baada ya waandamanaji kutawanya na hakukuwa na amri yoyote ya kutumia silaha dhidi ya Mwangosi,” alisema.


Baada ya kuahirishwa kwa kesi hiyo askari Polisi zaidi ya 30 waliokuwepo mahakamani hapo, walimchukua kwa kasi mtuhumiwa huyo na kumkimbiza katika magari mawili ya Polisi aina ya LandLover yaliyokuwepo mahakamani hapo na kutokomea naye huku wanahabari wakibuguziwa na baadhi yao wakizuiwa kumpiga picha mtuhumiwa huyo.

Reactions:

1 comments: