Saturday, 18 June 2016

Benki ya Dunia yaipa Tanzania fedha zaidi

Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia wa Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia, Bella Bird
MAISHA zaidi ya Watanzania milioni 6.6 walioko katika kundi la watu masikini na uhaba wa chakula yataboreshwa baada ya Benki ya Dunia kutoa nyongeza ya fedha za Dola za Marekani milioni 200 (sawa na bilioni 400 za Tanzania) kwa ajili ya miradi ya kuondoa umasikini.
Taarifa ya Benki ya Dunia kwa vyombo vya habari jana ilisema Bodi ya Wakurugenzi Watendaji imekubali kutoa msaada mpya kwa ajili ya programu zinazoendelea kwa ajili ya usalama wa jamii zinazotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Mradi wa Kaya Salama chini ya ufadhili wa TASAF, utasaidia mkakati wa Serikali ya Tanzania wa kuongeza misaada ya fedha bila masharti, sambamba na kuongeza ushiriki wa walengwa kufaidika kwenye programu mpya zinazohusisha kuboresha nguvu kazi kubwa ya umma, uwekaji akiba na vitegauchumi.
Desemba mwaka jana, mradi huo ulipata maendeleo makubwa kwa kufikia lengo la kaya milioni 1.1, au wastani wa watu milioni 6.6 miongoni mwa asilimia 15 ya watu masikini jumla ya idadi ya Watanzania milioni 45.
“Kuongezwa kwa kiwango hicho cha fedha katika kusaidia mtandao wa uzalishaji wa jamii salama kutaleta mageuzi makubwa katika mradi huo wa kusaidia kaya masikini Tanzania.,” alisema Bella Bird, Mwakilishi Mkazi wa Benki ya Dunia wa Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment