Thursday, 2 June 2016

BALOZI MAHIGA KUZINDUA MAKUMBUSHO YA IRINGA JUNI 25WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Dk Augustine Mahiga anatarajia kuizindua rasmi Nyumba ya Makumbusho ya Iringa, katika hafla itakayokwenda sambamba na maonesho ya rasilimali za utamaduni na historia ya mkoa wa Iringa.

Juzi, Katibu Mkuu wa Wizar ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof Elisante Ole Gabriel alitembelea nyumba hiyo iliyopo karibu na bustani ya manispaa ya Iringa na kupewa taarifa ya ukarabati wake unaofanywa kupitia mradi wa Kuendeleza Utamaduni Nyanda za Juu Kusini (Fahari Yetu) unaofadhiliwa na umoja wa nchi za Ulaya (EU).

Akizungumza na wanahabari meneja msaidizi wa mradi huo unaokishirikisha Chuo Kikuu cha Iringa (IUCo),  Jimson Sanga alisema nyumba hiyo itakayozinduliwa Juni 25, mwaka huu ilijengwa takribani miaka 116 iliyopita ikitumika kama boma la mjerumani ambayo baada ya Uhuru ikawa ofisi ya mkuu wa wilaya ya Iringa.

Katika uzinduzi huo, Sanga alisema utahudhuriwa pia na waziri wa maliasili na utalii, viongozi mbalimbali wa serikali, kimila na utamaduni, wananchi na washirika wa mradi huo ambao ni pamoja na makumbusho ya Taifa, shirika la Uhifadhiwa Wanyamapori (WCS), mradi wa SPANEST, Tanapa, Bodi ya Utalii Tanzania, shirika la kuendeleza watoto (CCDO), Chuo Kikuu cha Gottingen cha Ujerumani na Shirika la ACra-CCS.

Sanga alisema jengo hilo limefanywa makumbusho ya mkoa baada ya ofisi ya mkuu wa wilaya na watumishi wake kuhamia katika ofisi zake mpya katika eneo la Mawelewele, mjini Iringa zaidi ya miaka miwili iliyopita na baada ya wizara ya maliasili na utalii kuridhia litumike kwa matumizi hayo.


“Mradi huu wa utalii unahusisha ukarabati, uhifadhi na uhuishaji wa nyumba hiyo iliyokuwa boma ya Iringa enzi za utawala wa Kijerumani,” alisema na kuongeza kwamba boma hilo limekarabatiwa kwa zaidi ya Sh Milioni 240.

Alisema katika nyumba hiyo ya makumbusho kutakuwa na zana za asili zikiwemo zile zilizotumiwa kwa ajili ya chakula, kilimo, vita na ngoma za asili.

“Lakini pia kutakuwepo na taarifa mbalimbali za vivutio vya utamaduni vinavyoendelea kutambuliwa na vilivyotambuliwa likiwemo jiwe la Gangilonga la mjini Iringa linalodaiwa kuzungumza, michoro ya kale ya Igeleke na eneo lililotumiwa na wakoloni kuongea waharifu mjini Iringa la Kitanzini,” alisema.

Kwa upande wake Maneja wa Mradi wa Fahari Yetu, Jan Kuever alisema; “Mradi utashirikiana na wizara ya maliasili na utalii idara ya mambo ya kale, makumbusho ya Taifa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Iringa kuhakikisha makumbusho hiyo inapata hadhi inayokusudiwa.”

Lakini pia, Jan Kuever alisema, makumbusho hiyo itatoa huduma zingine kama ukumbi wa mikutano, mgahawa, duka la zawadi na itatoa mchango mkubwa kwa tafiti mbalimbali za utamaduni na historia ya mambo ya kale.

Alisema makumbusho hiyo itasaidia pia kuondoa umasikini katika jamii kwa kuziuza bidhaa za utamaduni katika soko la utalii.


Katibu Mkuu wa Wizar ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof Ole Gabriel amewataka mradi huo utakaoshirikiana na serikali kuiendesha makumbusho hiyo kuitangaza ndani na nje ya nchi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment