Monday, 6 June 2016

ALIYEBAKA NA KUMLAWITI MTOTO WA MIAKA SABA AFUNGWA JELA MAISHA


MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Iringa, imemhukumu Erick Msemwa (35) mkazi wa Mkimbizi, Iringa Mjini kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na makosa ya kubaka na kumlawiti mtoto wa miaka saba.

Msemwa aliyeshitakiwa katika mahakama hiyo kwa makosa matatu tofauti ya ubakaji na ulawati aliyotuhumiwa kuyatenda kati ya Januari na Februari mwaka 2015, alifikishwa kwa mara ya kwanza katika mahakama hiyo, Machi 4, 2015.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Andrew Scout baada ya kuridhishwa na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka uliokuwa na mashahidi nane.

Wakati upande wa mashtaka uliongozwa na waendesha mashtaka Hope Masambo na Happines Flavian, upande wa utetezi ulikuwa na mashahidi saba wakiwemo wazazi wa mshtakiwa huyo.

Katika shtaka la kwanza, Scout alisema Msemwa analishtakiwa kuzini na ndugu yake wa damu kati ya Januari na Februari, 2015kinyume na kifungu cha 158 (1) (a) cha sheria ya kanuni ya adhabu.

“Baada ya kuridhishwa na ushahidi wa upande wa mashtaka na muhukumu Msema kwenda jela miaka 30,” alisema wakati akitoa hukumu ya shtaka la kwanza.

Katika shtaka la pili Msemwa alihukumiwa kwenda jela maisha baada ya ushahidi wa upande wa mashtaka kuthibitisha bila shaka yoyote kwamba alifanya ngono na mtoto huyo kinyume na maumbile  kinyume na kifungu 154 (1) na (2) cha  sheria ya kanuni ya adhabu kama kilivyorekebishwa katika kifungu cha 185 na kifungu 119 (1) na (2) cha sheria ya watoto No 21 ya mwaka 2009.

Pamoja na adhabu hizo, mahakama hiyo ilimuhuku Msemwa kwenda jela miaka mitano kwa kosa la kumsababishia maumivu ya mwili mtoto huyo kinyume na kifungu 241 cha kanuni ya adhabu na hivyo atazitumikia adhabu hizo kwa pamoja.

Katika utetezi wake,  mtuhumiwa aliiomba mahakama hiyo bila mafanikio yoyote apunguziwe adhabu kwakuwa familia yake inamtegemea.

Awali Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Happines Flavian alisema hakukuwa na kumbukumbu za makosa ya nyuma dhidi ya mshtakiwa, hivyo aliiomba mahakama hiyo kutoa adhabu kwa mtuhumiwa kwa mujibu wa sheria ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.

Akizungumza na wanahabari mara baada ya hukumu hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela alisema; “hukumu hiyo imefungua ukurasa mpya wa namna ya kukabiliana na makosa ya ubakaji yanayozidi kushamiri wilayani Iringa.”

Kasesela alisema rekodi zinaonesha baadhi ya kesi za ubakaji na ulawiti zimekuwa zikiishia kwenye madawati ya uchunguzi Polisi na kutupiliwa mbali mahakamani baada ya kukosekana kwa ushahhidi.

“Matarajio yetu ni kuona vyombo vyote vya dola na mahakama vinashirikiana vyema ili kuzishughulikia kesi za aina hii kwa mujibu wa sheria ili kuyamaliza matukio haya,” alisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment