Wednesday, 18 May 2016

ZENGWE LADAIWA KUTUMIKA KUIFUNGA HOTELI YA KITONGA, WANAONUFAIKA WAPANGA KUANDAMANA
ZAIDI ya wananchi 2,500 wa kijiji cha Mahenge wameahidi kuandamana hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Kilolo wakipinga uamuzi wa halmashauri ya wilaya hiyo ya kuifungia kwa muda usiojulikana hoteli ya Kitonga Starcom, iliyopo katika mlima wa Kitonga, wilayani humo.

Kufungwa kwa hoteli hiyo kwa zaidi ya wiki mbili sasa, kumeelezwa na wananchi hao waliokuwa wakiitegemea kuuza mazao ya kilimo kuathiri biashara zao na maisha yao ya kawaida hali inayosababisha washindwe kumudu baadhi ya mahitaji yao ya kila siku.

“Tunachojua sisi hoteli hii inapigwa vita ya kibiashara na baadhi ya washindani wenzake wanaofanya biashara ya huduma za vyakula kwa abiria wanaosafiri katika ya Dar es Salaam na mikoa ya kusini,” alisema.

Mmoja wa waathirika aliyejitambulisha kwa jina la Mama Irine alisema; “mimi pamoja na wenzangu ni wajasiriamali tuliokuwa tunauza nyanya na vitunguu hotelini hapa na kwa abiria wa mabasi yanayosimama hapa. Sielewi kwa uamuzi huu wanataka akina mama na vijana wengine wanaoitegemea kupata vipato, wafanye ninini.”

Naye Maulid Mbugi alisema maamuzi hayo yamewakasirisha wananchi wengi wa kijiji hicho hatua inayowalazimu kuandamana hadi kwa mkuu wa wilaya kupeleka kilio chao.

“Hatutaki vijana wanaoitegemea hoteli hii wajiingize kwenye vitendo vya ujambazi na akina dada wajiingize kwenye vitendo vya ngono. Tunaomba serikali ifungue hoteli hii kwasababu dosari zinazotajwa zinaweza kurekebishwa wakati ikiendelea kutoa huduma,” alisema.

Meneja wa hoteli hiyo, Michael George alisema; “mbali na kuwaathiri wananchi walio jirani nayo, kufungwa kwa hoteli hiyo kumewaathiri pia wafanyakazi wa hoteli hiyo na familia zao.”

Akizungumzia uamuzi wa halmashauri ya wilaya hiyo kuifunga hoteli hiyo, Mkurugenzi wa hoteli hiyo, Henry Vegula alisema; “tuliopokea kwa mikono mwili pamoja na kwamba marekebisho yanayotajwa tungeweza kuyafanya wakati tukitoa huduma ili wananchi, wafanyakazi na wateja wetu wasiathirike.”

Alisema pamoja na uamuzi wake, tayari uongozi wa hoteli hiyo umekwishafanya marekebisho mbalimbali muhimu kama ilivyoelekezwa na halmashauri hiyo na akaomba serikali iwafungulie ili waendelee kutoa huduma.

Kwa mujibu wa barua ya Afisa Afya wa Wilaya ya Kilolo, Fanuel Nyadwike, hoteli hiyo imefungwa baada ya timu ya idara ya afya ya halmashauri hiyo kufanya ukaguzi Machi 22, mwaka huu na kunaini ikiwa na mapungu mbalimbali.

Mapungufu hayo kwa mujibu wa barua hiyo yenye  Kumb Na. KDC/H2/11/16 ni pamoja na uchakavu wa sakafu, kuta, paa na mitaro ya maji katika eneo la jiko.

Mengine ni masinki ya choo, vigae katika meza za jikono na eneo la utekeketezaji taka ngumu ambalo awali lilikuwa limejaa na halifai kuendelea kutumika.

Katika kuiboresha zaidi hoteli hiyo, Vegula alisema mipango yao ni pamoja na kuboresha mfumo mzima wa maji taka kwa kuzingatia kanuni na sheria za mazingira.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment