Saturday, 7 May 2016

Zanzibar yasisitiza ushirikiano na JapanRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein, amesisitiza haja ya kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Tanzania na Japan.
Alisema hiyo inatokana na taifa hilo kutambua hatua za nchi hiyo za kuendelea kuiunga mkono Tanzania katika kuimarisha miradi mbalimbali ya maendeleo.
Dk Shein alisema hayo jana Ikulu mjini Zanzibar, wakati alipozungumza na Balozi mpya wa Tanzania nchini Japan, Mathias Chikawe.
Katika mazungumzo hayo Dk Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Tanzania ikiwemo Zanzibar, inajivunia uhusiano na ushirikiano mzuri pamoja na hatua za Japan za kuendelea kuiunga mkono katika kukamilisha miradi kadhaa ya maendeleo hapa nchini.
Alisema Serikali ya Japan pamoja na Shirika lake la Maendeleo la Jica, kwa muda mrefu zimekuwa zikiunga mkono uimarishaji wa miradi ya maendeleo hapa nchini, ambapo kwa upande wa Zanzibar nchi hiyo imesaidia mradi mkubwa wa maji katika Mkoa wa Mjini Magharibi, ambao hivi sasa upo katika awamu ya tatu.
Dk Shein pia alitumia fursa hiyo kumueleza Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuitangaza zaidi Tanzania kiutalii kutokana na kuweko vivutio kadhaa kama fukwe nzuri za bahari kwa Zanzibar na hifadhi za Taifa kwa Tanzania Bara.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment