Wednesday, 18 May 2016

Yanga uwanjani leo

LEO ni fursa nzuri kwa Yanga kung’ara kimataifa wakati itakapokuwa mjini Dundo, Angola katika mchezo wa Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) dhidi ya Sagrada, Esperanca ya huko.
Yanga tayari ipo mjini Dundo, mji ambao upo umbali wa kilometa 1,300 kutoka Mji Mkuu wa Angola, Luanda.
Umbali huo ni sawa na kutoka Dar es Salaam hadi Bukoba kwa basi, lakini Yanga ilisafiri kwa ndege mpaka kwenye mji huo, ambao ni maarufu kwa uchimbaji wa madini ya dhahabu.
Kwenye mechi ya mkondo wa kwanza waliyoanzia nyumbani jijini Dar es Salaam, Yanga waliwafunga Sagrada Esperanca wa Angola kwa mabao 2-0, yaliyokuja kupatikana kipindi cha pili baada ya Waangola hao kubana sana kipindi cha kwanza, wakiegesha basi lao golini.
Lilikuwa bao zuri la Simon Msuva aliyefunga kwa kichwa kufuatia majalo ya chini chini ya Geoffrey Mwashiuya, akawaamsha viti mashabiki wa vijana hao wa Jangwani.
Bao jingine lilifungwa na chipukizi Matheo Anthony kwa mkwaju mkali. Sasa Yanga wanajiwinda kwa mechi ya mkondo wa pili leo, na wanatakiwa kutopoteza kwa zaidi ya bao moja ili wasonge mbele.
Kwa maana nyingine, Yanga wanaofundishwa na Mholanzi Hans Pluijm wakishinda kwa idadi yoyote ya mabao leo, kwenda sare kwa idadi yoyote au hata kufungwa bao moja tu, watakuwa wamevuka na kuingia hatua ya makundi.
Kwa maneno mengine ni kwamba hatima yao imo mikononi mwao wenyewe, washindwe tu kutumia fursa itakayokuja wakiwa tayari wamekabidhiwa mwali wa Ligi Kuu Tanzania mwishoni mwa wiki walipocheza na Ndanda. Kocha Mkuu wa Yanga, Pluijm amesema Yanga wana kazi bado mbele inawakabili na wana imani kwamba ndoto zake zitafanikiwa.
Pluijm anaweza kuwa na sura nne ambazo hazikucheza mchezo wa kwanza ambazo ni Haji Mwinyi, Vincent Bossou, Thabani Kamusoko na mshambuliaji mahiri, Donald Ngoma.
Uwepo wa wachezaji hao wenye uzoefu mkubwa na mashindano ya kimataifa ni faraja kubwa kwa Pluijm, anayejiwinda kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kutoka Tanzania kuingia hatua ya makundi ya mashindano hayo.
Ngoma ndiye mfungaji wa bao pekee la Yanga kwenye mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al Ahly uliochezwa Alexandria Misri na Yanga kutolewa kwa mabao 2-1.
Yanga haitakuwa na mshambuliaji wake Malimi Busungu aliyeumia kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam, lakini timu hiyo ina utajiri katika eneo hilo kwani itakuwa na mfungaji wa bao la pili, Antony Mateo au Paul Nonga.
Sagrada Esperanca hawakuonesha uwezo wao kwenye mchezo wa kwanza, kwani ilicheza soka la kujihami la kutafuta sare ama hata kama ikifungwa iwe idadi ndogo ya mabao, hivyo wakiwa nyumbani wanaweza kuwa hatari kwa Yanga leo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment