Saturday, 7 May 2016

Wanaopeleka mahujaji Makka wapewa angalizo

SHIRIKISHO la Taasisi za Hijja nchini (TAHEFA) imezitaka taasisi zinazopeleka mahujaji Makka kuhiji kufuata muongozo uliotolewa na Wizara ya Hijja ya Saudi Arabia, huku likionya kuzichukulia hatua kali taasisi ambazo zitakwenda kinyume na taratibu.
Aidha, taasisi za Hijja 31 zimeruhusiwa kupeleka mahujaji Saudi Arabia kwa ajili ya ibada hiyo mwaka huu baada ya kukidhi vigezo vilivyowekwa na wizara hiyo.
Hatua ya kuzichukulia hatua taasisi hizo inatokana na moja ya taasisi za hapa nchini zinazopeleka mahujaji Makka kwa ajili ya ibada ya Hijja, iliyotajwa kama Markaz Shamsiya kushindwa kuwapeleka mahujaji hao licha ya kulipa fedha.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Mwenyekiti wa shirikisho hilo Tanzania Bara, Shehe Abdallah Khalid alisema, kitendo hicho kiliwasikitisha na tayari wameshachukua hatua za kuifungia taasisi hiyo kusafirisha mahujaji.
Alisema kwa sasa shirikisho hilo lina kamati ya nidhamu ambayo itakuwa ikiziwajibisha taasisi ambazo zitaonekana kwenda kinyume na taratibu.
“Hili jambo lilitupa huzuni sana kusikia mahujaji wamelalamika, walilipa fedha zao halafu hawakwenda kufanya ibada ya Hijja… tulifanya ufuatiliaji na hatua tulizochukua ni kuifungia isisafirishe mahujaji,” alisema Khalid.
Aidha, alisema shirikisho hilo linaangalia uwezekano wa kuweka bei elekezi kutokana na kuwepo kwa baadhi ya taasisi kutoza bei ya chini lakini zinawapeleka mahujaji mbali zaidi na misikiti na kutotoa huduma zote.
Khalid alisema kila taasisi ili iweze kukidhi vigeze ni lazima mahujaji wote wasajiliwe na kuingiza taarifa zao kulingana na hati zao za kusafiria kupitia mtandao ili kuwawezesha kupata huduma ikiwemo Viza kabla ya Julai 20, mwaka huu.
“Lakini pia taasisi zote zinatakiwa kuingia mikataba rasmi ya huduma zote kupitia mtandao kwa mawakala, mashirika nakampuni zilizosajiliwa na Wizara ya Hija kutoa huduma hizi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment