Sunday, 8 May 2016

WAMILIKI WA GUEST DAR WATAKIWA KUFUNGA KAMERA ZA CCTV


Kufuatia matukio kadhaa ya uhalifu ikiwemo mauaji yanayofanywa katika nyumba za kulala wageni, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita amependekeza ufungwaji wa kamera maalum za CCTV katika nyumba hizo ili kuimarisha ulinzi.

Amesema mamlaka husika wakiwemo wamiliki wa gesti na hoteli wanapaswa kuliangalia suala hilo kwa jicho la tatu ikiwa ni siku chache zimepita tangu kuripotiwa tukio la kufariki mwanamke mmoja akiwa gesti Jijini Dar es Salaam.

“Kamera hizi hazitafungwa vyumbani bali zifungwe maeneo ya nje ya gesti au hoteli husika, mapokezi kwani hii ndio itakuwa njia sahihi ya kupambana na matukio ya kihalifu kama haya na kuwabaini wahalifu,” ameongeza Meya Mwita.

Amewataka pia viongozi wa dini wa Mkoa wa Dar es Salaam kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili wakazi wa Jiji hilo waweze kumrudia Mungu na kuachana na vitendo vya kinyama.


Wakati huohuo, Meya Mwita amekanusha vikali taarifa zilizosambaa katika mitandao ya kijamiii kuwa ameagiza wamiliki wa gesti na hoteli kuwapiga picha wageni wanaokwenda kulala katika nyumba hizo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment