Wednesday, 18 May 2016

VIWANJA VYA UVCCM IRINGA VYAWASHA MOTO, VIONGOZI WAWILI WATIWA MBARONI

Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Sadifa Hamis Juma.

KAIMU Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa, Elisha Mwampashi ambaye pia ni Katibu wa CCM Manispaa ya Iringa na aliyekuwa Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Iringa, Alli Nyawenga wametiwa mbaroni wakituhumiwa kuuza baadhi ya viwanja, mali ya UVCCM mkoa wa Iringa, tuhuma ambazo wote wawili wamekana kuhusika nazo.

Akizungumza na wanahabari jana, Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, John Kauga alisema wawili hao wameshitakiwa na Tume ya Uchunguzi ya Baraza la Wadhamini la UVCCM Taifa.

Wakati Nyawenga alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita mkoani Morogoro na kuletwa mjini hapa Jumapili, Mwampashi alikamatwa Jumatatu na wote wawili wakafikishwa mahakamani juzi, Jumanne na kutolewa magereza jana baada ya kukamilisha taratibu za dhamana.

Alisema taarifa za awali zinazoendelea kuchunguzwa na jeshi la Polisi zinaonesha watuhumiwa hao walihusika na uuzaji wa viwanja hivyo vilivyopo katika eneo la Igumbiro, mjini Iringa.

“Mchakato wa biashara ya viwanja hivyo ambavyo hata hivyo idadi yake haijawekwa wazi, ulifanyika kati ya Machi na Desemba, mwaka jana,” alisema.

Kauga alisema baada ya kupokea taarifa hiyo na kuwashikilia watuhumiwa hao hao wawili, Jeshi la Polisi kwa maelezo linayoendelea kuyapata kutoka katika baraza hilo la wadhamini, unaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho na zilizothibitishwa na mmoja wa viongozi wa chama hicho (hakutaka kutaja jina kwa kuwa sio msemaji) zinasema UVCCM Mkoa wa Iringa walikuwa wakilimiliki shamba lenye ukubwa wa heka 210 katika eneo hilo.

“Kwa kuwa sheria za miji haziruhusu kuwa na shamba la ukubwa huo mjini, UVCCM walifanya mchakato wa kubadilisha matumizi, kutoka kwenya shamba ili pawe na viwanja kwa matumizi mbalimbali,” alisema.

Ili wafanikishe azma hiyo, alisema UVCCM waliamua kuuza sehemu ya shamba hilo ili fedha zitakazopatikana zisaidie kuharakisha mchakato wa upimaji wa vianjwa katika shamba hilo.

“Kwahiyo tunasikia zikauzwa heka 30 kwa mfanyabiashara mmoja wa kiasia wa mjini hapa kwa kiasi kinachokadiriwa kufika Sh Milioni 90,” alisema.

Alisema sehemu ya fedha hizo zilitumika kufanikisha shughuli ya upimaji wa viwanja hivyo kwa kushirikiana na idara ya ardhi ya halmashauri ya manispaa ya Iringa.


“Katika heka 180 zilizobaki, vilipatikana viwanja 185 baada ya upimaji wa viwanja hivyo kukamilika, viwanja ambavyo baadhi yake  vinadaiwa kuuzwa,” alisema na kuongeza kwamba hajui kama kweli viliuzwa na kwa kuzingatia utaratibu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment