Sunday, 22 May 2016

UTULIVU WAPOTEA CHADEMA IRINGA, MWENYEKITI WA JIMBO ASIMAMISHWA


HALI si shwari ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Iringa Mjini baada ya jana kamati tendaji yake kufanya maamuzi magumu yaliyomsimamisha, mwenyekiti wa chama wa jimbo hilo, Frank Nyalusi kuendelea na wadhifa wake huo.

Pamoja na Nyalusi, kamati hiyo inayoundwa na wajumbe 21 iliyohudhuriwa pia na mbunge wa jimbo hilo, Mchungaji Peter Msigwa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Suzan Mgonakulima imetengua uteuzi wa Diwani wa Kata ya Gangilonga, mjini hapa, Dady Igogo kuendelea kuwa mjumbe wa kamati hiyo.

Wawili hao, wamesimamishwa kuendelea na nyadhifa zao hizo ikiwa ni siku kadhaa tangu mtandao huu kuwaripoti wakimtuhumu Mstahiki Meya wa Manispaa ya Iringa, Alex Kimbe anayetokana na chama chao kuendesha vikao vya baraza la madiwani kibabe na kwa upendeleo.

Taarifa za kusimamishwa kwa viongozi hao ambazo viongozi wa chama hicho wamesema hawawezi kuzizungumzia kwa kina kwasababu zinahitaji maamuzi ya mwisho ya mkutano mkuu wa jimbo, zilisambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii hii leo.

Akizungumza na mtandao huu huku akikwepa kutoa taarifa ya maamuzi hayo moja kwa moja, Mgonakulima ambaye pia ni katibu wa chama wa jimbo hilo alisema; “Jana Mei 21 tulikaa kamati tendeji iliyojadili mwenendo wa chama katika jimbo letu na kufanya maamuzi yatakayopelekwa kwenye mkutano mkuu.”

Mgonakulima alisema maamuzi hayo hata kama yapo kwenye mitandao ya kijamii yataendelea kuwa siri ya chama hicho hadi pale mkutano mkuu utakapokutana na kuyabariki au kuyakataa.

“Mimi ni katibu kweli lakini siwezi kutoa taarifa yoyote ya kikao hicho cha kamati kwasasa kwenye vyombo vya habari mpaka nipate ridhaa ya chama,” alisema huku akisisitiza maamuzi yaliyofanywa na kikao hicho ni ya siri.

Akizungumzia taarifa ya kusimamishwa kwake uenyekiti, Nyalusi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Mivinjeni mjini Iringa alisema; “nimepata taarifa hizo kupitia kwa baadhi ya wajumbe waliohudhuria kikao hicho ambacho sielewi kilikuwa ni kikao gani kwasababu hakikuitishwa na mimi kama mwenyekiti baada ya kushauriana na sekretarieti yangu ya chama.”

Nyalusi alisema katika mazingira ya kushangaza alialikwa katika kikao hicho ambacho hakujua kama ni cha kamati tendaji kwa njia ya ujumbe wa maandishi mafupi kwa kupitia simu yake ya kiganjani.

“Nilipofika katika chumba cha mkutano, nikakaribishwa ili nifungue kikao hicho, nikauliza hiki ni kikao gani, nikaelezwa ni cha kamati tendaji. Nilishangaa na kuuliza kinawezaje kuitishwa bila kufuata taratibu, sikupata jibu la kueleweka,” alisema.

Alisema baada ya kukosa jibu alikataa kukifungua kikao hicho alichokiita ni cha uasi ndani ya chama na kuondoka zake bila kusaini daftari la mahudhurio ili kujiepusha na uvunjaji wa katiba.

Nyalusi anayefahamika mjini hapa kwa ujasiri mkubwa wa kusigana na viongozi wa serikali na vyombo vya dola alisema atachukua hatua za haraka kwa mujibu wa katiba ya chama chao pindi atakapopewa rasmi barua ya kusimamishwa madaraka yake hayo.

Kwa upande wake Igogo aliyetenguliwa kuendelea kuwa mjumbe wa kamati tendaji hakuweza kupatikana kuzungumzia taarifa hizo pamoja na kuwepo kwa taarifa zisizo rasmi katika mitandao ya kijamii zinazoonesha alikwishajiuzulu nafasi hiyo kutokana na kutingwa na majukumu yake mengine.

Siku moja kabla kikao hicho hakijafikia maamuzi ya kuwaadhibu viongozi hao,  Mchungaji Msigwa ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa alisema baadhi ya madiwani wa chama hicho wana utovu wa nidhamu unaohatarisha maslai ya chama na wananchi wa jimbo hilo.

Msigwa aliyasema hayo alipokuwa akizungumzia taarifa za baadhi ya madiwani kumtuhumu mstahiki meya wa manispaa ya Iringa kwa ubabe na upendeleo.

“Kwenye chama chetu hakuna mtu aliye juu ya chama. Ni lazima viongozi waliochaguliwa waheshimiwe, ni kosa kiongozi akamtukana kiongozi mwenzake hadharani halafu akavumiliwa, ” alisema.


Alisema kuna watu wengi walijaribu kuwa juu ya chama wakashughulikiwa na wengine kufukuzwa hadi uanachama kwasababu huo ni uasi ndani ya chama.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment