Saturday, 7 May 2016

Ummy: Serikali kujenga vyumba vya upasuaji kuokoa wajawazitoSERIKALI imepanga kujenga vyumba vya upasuaji vya dharura katika vituo vyote vya afya ili kupunguza vifo vya wajawazito nchini.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu wakati wa mkutano na wadau mbalimbali wa masuala ya wanawake na wasichana katika kujadili mapendekezo yatakayopelekwa katika mkutano wa Dunia kuhusu usawa wa jinsia na maendeleo ya wanawake utakaofanyika nchini Denmark.
Mkutano huo uliwashirikisha mfumo Afya na usimamizi (MST), Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP), Ubalozi wa Denmark nchini Tanzania, Chama cha wanawake wanasheria Tanzania (TAWLA), Tume ya Kudhibiti Ukimwi (TACAIDS), Marie Stopes Tanzania, Femina Hip na Wizara ya Afya, Jamii, Maendeleo, Jinsia na watoto.
Alisema kumekuwepo na ongezeko la vifo vya kina mama wajawazito nchini hivyo kuwepo kwa vyumba hivyo vya dharura kutasaidia kupunguza vifo hivyo.
“Serikali hii ya awamu ya tano ina mipango mizuri hasa kwa wanawake hivyo tumejipanga kuhakikisha Tanzania haina kifo cha mama mjamzito kwa kukosa huduma za dharura,” alisema.
Waziri Ummy alisema wizara hiyo imepata mafanikio katika kuweka haki ya afya ya uzazi, usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake katika ajenda ya maendeleo, kwani wanawake na wasichana bado wanajitahidi kudai huduma za haki. “Juhudi zaidi zinahitajika ili kutekeleza sheria na sera, mabadiliko ya mitazamo chanya kuhusu ndoa za utotoni na mimba za utotoni na afya ya uzazi ya wanawake kupatikana kwa haki,” alisema.
Kwa upande wake Balozi wa Denmark nchini Einar Jensen alisema mkutano huo utakaofanyika Mei 16 mpaka 29, mwaka huu utalenga kuangalia ni kwa njia gani utekelezaji wa agenda ya maendeleo endelevu ya 2030, unaohusu wasichana na wanawake na kujikita zaidi katika afya, hasa ya mama na uzazi na usawa wa kijinsia.
“Utafiti umetuonesha kuwekeza kwa wasichana na wanawake siyo kitu pekee cha kufanya, hivyo ni vyema kuwekeza zaidi ya mtu binafsi kwa mfano wanawake wanatumia asilimia 90 ya mshahara wao kwa ajili ya watoto kuhusu afya, elimu na ustawi wa familia yeye anatumia kati ya asilimia 30 na 40 tu,” alisema Jensen.
Aliongeza kuwa mkutano huo unatarajia kuwashirikisha wajumbe 5,000 kutoka katika nchi mbalimbali wakiwemo viongozi mbalimbali wa dunia, wasomi, watunga sera, wanaharakati , watu wa habari, dini vyama vya kijamii na wawakilishi wa sekta binafsi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment