Tuesday, 10 May 2016

SONGAS YAZIMA MITAMBO YAKE IKISHINIKIZA TANESCO IWALIPE DENI LAO


Kampuni ya kufua umeme kwa njia ya gesi asilia, Songas Limited imezima mitambo yake, baada ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushindwa kulipa deni la Sh193.5 bilioni, jambo linalotishia ukosefu wa nishati hiyo muhimu nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Songas, Nigel Whittaker amewaambia waandishi wa habari kuwa wameamua kuchukua hatua ya kuzima mitambo hiyo baada ya kuzidiwa na gharama za uendeshaji kutokana na deni hilo.

“Mtambo huo uliopo Ubungo unazalisha Megawati 189, tumefikia hatua ya kuzima kidogo kidogo kuanzia Aprili 29 mwaka huu kutokana na deni hilo, Tanesco imekuwa ikisuasua katika kulipa,” alisema Whittaker.

Alisisitiza kuwa mradi huo wa Songas ni muhimu kwa uchumi wa Tanzania na umekuwa ukizalisha umeme kwa kutumia gesi asilia kutoka Songosongo na kuuingiza katika gridi ya taifa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felchesmi Mramba, alisema Songas wamevunja makubaliano ya mkataba hususan kifungu cha 4.4 ambacho kinaitaka Songas kutoa siku 90 ya kuwa na majadiliano.

Mramba amewatoa wananchi hofu kuwa nchi haitaingia gizani  licha ya Songas kutangaza kuzima kabisa mitambo yote.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment