Saturday, 7 May 2016

Shule binafsi wasema ada elekezi yatishia elimu

 

Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako

SHIRIKISHO la wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali Tanzania (TAMONGSCO) limesema ipo haja kwa serikali kutangaza ada elekezi mapema ili kuondoa utata uliopo unaotishia kukwamisha maendeleo ya elimu.
Shirikisho hilo limesema kwamba mambo mengi ya maendeleo katika shule hizo yamekwama kutokana na kusubiri ada elekezi.
Akizungumza kumkaribisha Waziri wa Elimu,Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, katika mkutano wa shirikisho hilo mjini hapa, Mwenyekiti wa Shirikisho Mrinde Mzava, alisema walifurahishwa na kufika kwake Waziri, kwani waliamini kupata maelekezo ya ada elekezi ili kumaliza shida zilizopo sasa za uendeshaji.
Alisema mwenyekiti huyo kwamba kuna hatari katika elimu kama hali ya ucheleweshaji wa uchambuzi wa gharama za ada elekezi itaendelea.
Alisema pamoja na serikali kukiri kuwa suala hilo lipo mezani kwa ajili ya mazungumzo, hivi sasa shule na vyuo binafsi vimejikuta vikiweka viwango visivyotakiwa kisheria ambapo kwa upande wao kuna madhara makubwa.
Mwenyekiti huyo alisema kutokana na suala la ada elekezi kuwa kwenye mazungumzo wanaiomba serikali iliangalie kwa haraka ili lipunguze mzigo wa gharama za uendeshaji na ukubwa wa ada kwa lengo la kufanikisha utoaji wa elimu bora.
Katika mkutano huo serikali imeelezea kusikitishwa kwake na baadhi ya shule na vyuo kugeuza elimu kama sehemu ya kufanyia biashara. Aidha imesema kuwa bado haijapitisha ada elekezi kwa wamiliki wa shule na vyuo vya watu binafsi kutokana na jambo hilo kuwa kwenye meza ya mazungumzo kati serikali na wamiliki hao.
Kauli hiyo ambayo imetolewa na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Prof Joyce Ndalichako, wakati wa ufunguzi wa mkutano mkuu wa mwaka wa shirikisho la wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali Tanzania (TAMOMGSCO) mjini Dodoma.
Alisema baadhi ya shule na vyuo hivyo binafsi hivi sasa wakati majadiliano kuhusu ada elekezi yanaendelea, wamiliki wake wameweka maslahi zaidi ya kibiashara na kuwaumiza wananchi na wizara kamwe haitavumilia.
Alisema Wizara yake inasisitiza wamiliki kufuata miongozo ya serikali, na wale ambao hatawafuata haitawavumilia. Waziri Ndalichako alilazimika kutoa ufafanuzi huo kutokana na shirikisho hilo kutaka kufahamu kuhusu ada elekezi na kutaka kupatiwa maelekezo kutoka serikalini juu ya shule na vyuo binafsi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment