Saturday, 14 May 2016

Shombo ya samaki marufuku mabasi ya kasi Dar

 
ABIRIA wenye mizigo mikubwa na samaki wasiohifadhiwa vizuri, hawataruhusiwa kupanda mabasi yaendayo haraka jijini Dar es Salaam.
Hatua hiyo imelenga kuwapunguzia bugudha na shombo watumiaji wengine wa vyombo hivyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni inayoendesha mabasi hayo UDA-RT, David Mgwasa, aliyasema hayo alipozungumza na gazeti hili jana, alipoulizwa kuhusu abiria wanaosafiri na samaki kutoka Kituo cha Kivukoni kwenye Soko la Kimataifa la Samaki na kwingineko.

Alisema ili kuepuka abiria wengine kubugudhiwa na kupata shombo ya samaki, abiria wenye mizigo mikubwa hawataruhusiwa na wenye samaki lakini watakaohifadhi samaki vizuri kwenye ndoo safi, watatumia huduma hiyo.
UDA-RT ilianza kutoa huduma ya usafiri kwa mabasi hayo kuanzia Jumanne wiki hii na inaendelea kusafirisha abiria bure hadi Jumapili, lengo likiwa ni kutoa muda wa elimu ya namna ya kutumia mabasi hayo.
Aidha, Mgwasa alisema leo mabasi hayo yataanza saa 12 asubuhi mpaka saa tano usiku.
Alisema kuwa wamekuwa wakiongeza muda zaidi nyakati za usiku, kutokana na changamoto za nyakati hizo, kabla ya kuanza rasmi huduma hiyo Jumatatu.
Kwa mujibu wa Mgwasa, kwa sasa kuna mabasi 80 barabarani katika njia zote. Kesho kutwa, Jumapili, UDA-RT itahakikisha mabasi yote 140 yanakuwa barabarani, kufanya majaribio ya kubadilisha abiria.
“Tunazidi kuongeza muda wa kulaza mabasi, na pia Jumapili tutatoa mabasi yote, kwani mbali na kuangalia suala zima la abiria na uendeshaji pia tunaangalia namna nzuri ya madereva kubadilishana, maana haiwezekani dereva akaamka saa 10 aendeshe hadi usiku,” alisema.
Uwezo wa magari Mgwasa alisema mabasi makubwa yana uwezo wa kubeba abiria 150 kwa safari moja na madogo yanabeba abiria 90.
Wingi wa watu unaoonekana kwenye mabasi hayo kwa sasa, unatokana na kuruhusu mabasi machahe kuwa barabarani. Kadi (tiketi) Mgwasa alisema kadi maalumu ambazo zitauzwa kwa Sh 5,00 kwa bei ya promosheni, itakuwa ikitumika kwa mtu mmoja wakati wa safari.
“ Mtu kama ana kadi moja na anasafiri na familia yake, kadi hiyo itatumika kwa mtu mmoja na wengine watalazimika kukata tiketi, kwani kadi itamruhusu mtu mmoja wakati wa kuingia na kutoka,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment