Tuesday, 24 May 2016

SARAKASI ZAENDELEA KUPIGWA CHADEMA IRINGA MJINI, MWENYEKITI AGOMA KUACHIA NGAZI


MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Jimbo la Iringa Mjini, Frank Nyalusi aliyesimamishwa kuendelea na madaraka hayo, amejitokeza hadharani na kusema hatambui uamuzi huo batili.

“Mimi ni mwenyekiti halali, nilichaguliwa kwa kuzingatia katiba ya Chadema na nitaondoka madarakani kwa kuzingatia katiba hiyo hiyo na wala si kwa vikao feki,” alisema alipokuwa akipinga maamuzi yaliyofanywa na Kamati Tendaji ya jimbo hilo dhidi yake.

Hivi karibuni, kamati tendaji ya jimbo hilo iliyoketi Mei 21, mwaka huu ilifanya a maamuzi magumu yaliyomsimamisha Nyalusi kuendelea kuhudumu katika chama hicho kwa kupitia nafasi hiyo.

Kwa kupitia barua ya chama hicho iliyosainiwa na Katibu wa jimbo hilo, Suzan Mgonakulima ambayo hata hivyo haikuwa na kumbukumbu namba, Nyalusi amesimishwa uongozi wa chama hicho akituhumiwa kufanya matendo mbalimbali yanayokidhalilisha chama.

“Katika kikao chake cha kamati ya utendaji kilichokaa Mei 21, 2015 kimepokea malalamiko kutoka vyanzo mbalimbali ndani na nje ya chama huku kamati ikijiridhisha yenyewe kuwa matendo mbalimbali ambayo umekuwa ukiyafanya, ynakidhalilisha chama hivyo kuona kuwa unakosa sifa ya kuendelea kuwa kiongozi mkuu wa chama katika manispaa ya Iringa,” inasomeka sehemu ya barua hiyo aliyokabidhiwa mwenyekiti huyo.

Barua hiyo inaendelea kusomeka “kwa kupitia barua hii unaarifiwa kusimama kufanya majukumu yako kama mwenyekiti hapa jimboni mpaka mamlaka za kikatiba zilizo juu ya kamati ya utendaji zitakapotoa uamuzi wake.”

Aidha kwa kupitia barua hiyo, Chadema imesema chama hakijasita kumpongeza kwa kazi kubwa na nzito aliyofanya Nyalusi kwa kipindi kilichopita hadi wakapata ushindi mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Akipuuza barua hiyo ya kusimamishwa nafasi ya uongozi, Nyalusi ambaye pia ni diwani wa kata ya Mivinjeni Iringa Mjini alisema; “pamoja na kwamba kilikuwa batili, kikao hicho hakina mamlaka yakufanya maamuzi ambayo kimsingi yanatakiwa kufanya na mkutano mkuu wa jimbo.”

Nyalusi anayeungwa mkono na baadhi ya wanachama wanaopinga maamuzi ya kamati hiyo alisema ataendelea kuwa mwenyekiti wa chama hicho akitekeleza majukumu yake ya uenyekiti mpaka pale vikao halali vya kikatiba vitakapotoa maamuzi yake.

“Niwaombe wanachama wawe watulivu na wapuuze maamuzi ya kikao batili cha kamati tendaji kilichoketi kwa shinikizo la viongozi fulani, mimi ni mwenyekiti wao na nitaendelea kuwa mwenyekiti mpaka pale vikao halali vya chama vitakapoamua vinginevyo,” alisema.

Akikizungumzia kikao kilichomsimamisha uenyekiti, Nyalusi alisema; “nilipata taarifa za kikao hicho kupitia simu yangu ya kiganjani, yaani ni jambo la kushangaza sekretarieti inaitisha kikao kama hicho bila kushauriana na mwenyekiti na baadae mwenyekiti anaalikwa tena kwa ujumbe mfupi wa simu ya mkononi, kwa mujibu wa katiba yetu hilo ni kosa kubwa.”

“Nilipofika katika chumba cha mkutano, nikakaribishwa ili nifungue kikao hicho, nikauliza hiki ni kikao gani, nikaelezwa ni cha kamati tendaji. Nilishangaa na kuuliza kinawezaje kuitishwa bila kufuata taratibu, sikupata jibu la kueleweka,” alisema.

Alisema baada ya kukosa jibu alikataa kukifungua kikao hicho alichokiita ni cha uasi ndani ya chama na kuondoka zake bila kusaini daftari la mahudhurio ili kujiepusha na uvunjaji wa katiba.

Nyalusi anayefahamika mjini hapa kwa ujasiri mkubwa wa kusigana na viongozi wa serikali na vyombo vya dola alisema atachukua hatua za haraka kwa mujibu wa katiba ya chama chao pindi atakapopewa rasmi barua ya kusimamishwa madaraka yake hayo.

Pamoja na Nyalusi, kamati hiyo ilimvua ujumbe wa kamati tendaji, Diwani wa kata ya Gangilonga Dady Igogo ambaye naye anatuhumiwa kwa makosa yanayofanana na Nyalusi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment