Saturday, 7 May 2016

MSD waingia mkataba na mawakala 13BOHARI ya Dawa (MSD) imeingia mkataba na mawakala 13 wa ndani kwa ajili ya kusambaza dawa pale zitakapokosekana katika maghala ya bohari hiyo.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangallah alisema jana kuwa lengo la kuingia mkataba na mawakala hao ni kupunguza mlolongo mrefu wa ununuzi wa dawa kwa sasa.
“Mikataba hii itasaidia halmashauri kupata dawa katika muda mfupi…juhudi zinafanyika kuongeza idadi hiyo ili kuimarisha utoaji wa huduma za dawa nchini. Wizara yangu imewasilisha mapendekezo ya kufanya mapitio ya Sheria ya Manunuzi, ili dawa zinunuliwe kwa muda mfupi zaidi kuliko ilivyo sasa hivi,” alisema.
Dk Kigwangallah alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Itilima, Njalu Silanga (CCM), aliyetaka kufahamu Serikali imejipangaje kuboresha mfumo wa ununuzi ili kupunguza mlolongo mrefu wa ununuzi uliopo sasa wa halmashauri kutoa fedha kisha kusubiri mpaka MSD itafute mzabuni mwingine.
Kuhusu mgawo wa dawa unaotolewa kutoka MSD kwenda vituoni, alisema Serikali imetoa maelekezo kwamba vituo vyote vya umma vipatiwe dawa bila kujali kama vina deni MSD.
“Pale wizara inapopata mgawo wa fedha kutoka Hazina, madeni hayo hulipwa. Pia wizara yangu imeagiza halmashauri kutumia vyanzo mbadala vya mapato kama vile CHF, makusanyo ya papo hapo na fedha toka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) zitumike kununulia dawa ili kuziba pengo la bajeti toka Serikali Kuu,” alisema.
Alisema fedha nyingine ni za Mfuko wa Pamoja ambazo asilimia 67 inatakiwa itumike kununulia dawa, vifaa, vifaa tiba na vitendanishi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment