Wednesday, 18 May 2016

MPM MGOLOLO YASHITAKIWA SERIKALINI, YADAIWA KUIPOTEZEA SERIKALI MAPATO MAKUBWA
UMOJA wa Wavunaji Miti katika Shamba la Saohil (UWASA) wamekishitaki Kiwanda cha Karatasi cha Mgololo (MPM Mgololo) kwa Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo Makani, wakikituhumu kuipotezea serikali wastani wa Sh Bilioni 6 kila mwaka, toka mwaka 2006.

Waziri huyo alifanya ziara yake ya siku moja wilayani Mufindi juzi iliyomuwezesha kupata taarifa ya sekta ya maliasili na utalii, wilayani humo kabla hajakutana na wadau wa shamba la miti la Saohill na kusikiliza changamoto zao mbalimbali.

Akimuomba Rais Dk John Magufuli asaidie kushughulikia upotevu wa mapato hayo, Katibu wa umoja huo, Dk Basil Tweve alimwambia waziri huyo kwamba mwekezaji huyo amekuwa akinunua magogo katika shamba hilo la serikali kwa nusu bei, tofauti na bei elekezi inayotozwa kwa wavunaji wadogo.

“Ununuzi kwa nusu bei, umesababisha mapato mengine yanayotakiwa kulipwa na mwekezaji huyo serikalini kama kodi na ushuru kupungua na hivyo kuifanya serikali kukosa inachostahili kupata,” alisema.

Akifafanua jinsi serikali inavyopoteza mapato yake kwa kupitia mwekezaji huyo,  Makamu Mwenyekiti wa UWASA, Carlos Kinyoa alisema; “wakati wavunaji wadogo wanaotakiwa kujengewa mazingira rafiki na serikali wakilipa Sh 28,000 kwa mita moja ya ujazo ya gogo, wawekezaji hao ambao wanauziwa malighafi hiyo kwa nusu ya bei, wanalipa Sh 14,000.”

Katibu Msaidizi wa UWASA, Alex Ngogo alisema malipo hayo ni nje ya kodi mbalimbali wanazotakiwa kulipa kutoka katika mita za ujazo zaidi ya 200,000 wanazopewa kwa uvunaji kila mwaka ili kuendesha kiwanda chao.

“Mapato ya kodi hizo ambayo kimsingi yanapungua kwasababu ya kiwanda hicho kununua malighafi hiyo kwa nusu ya bei ni pamoja na ya Ongezeko la Thamani (VAT), ushuru wa halmashauri na kodi mbalimbali za uendeshaji wa msitu,” alisema Ngogo.

Alisema ni muhimu serikali ikafumua mikataba baina yake na mwekezaji huyo, kama ipo kisheria, ili naye anunua malighafi hiyo kwa kuzingatia bei elekezi inayotumiwa na wawekezaji wadogo.

Akiahidi kulishughulikia suala hilo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Makani alisema watahitaji kupitia mikataba na mwekezaji huyo, kutembelea kiwanda na kumsikiliza kabla ya kuja na suluhisho la mgogoro huo wa uvunaji.

“Lazima nikiri kwa taarifa nilizonazo hata kabla sijaja hapa, kuna matatizo makubwa kwenye utaratibu wa uvunaji wa miti, lakini matatizo hayo yapo pia kwenye masoko na viwanda vya mbao ambayo tunatakiwa kuyakabili,” alisema.

Kiwanda cha MPM Mgololo kilibinafsishwa mwaka 2004 kwa makampuni ya Rai ya nchini Kenya kwa Dola za Kimarekani Milioni moja baada ya kusimama kufanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 kwasababu mbalimbali ikiwemo ya ukubwa wa gharama za uendeshaji.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment