Wednesday, 18 May 2016

MADIWANI WA CHADEMA WAMTUHUMU MEYA WAO KWA UBABE, WATAKA AITWE VIKAONIMSTAHIKI Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe yupo katika hatari ya kukalia kaa la moto baada ya baadhi ya madiwani kutoka katika chama chake Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kinachounda halmashauri hiyo kumtuhumu kuendesha vikao vya baraza la madiwani kibabe.

Katika kikao cha baraza la madiwani kilichoketi jana mjini Iringa, Kimbe alisisitiza kwa madiwani wote wakiwemo wa chama chake kuzingatia kanuni wakati wa vikao hivyo ili haki itendeke.

Mara kadhaa meya huyo aliwaamuru kutoendelea kuzungumza baadhi ya madiwani, wengi wao kutoka katika chama chake, waliotaka kuuliza au kuchangia hoja mbalimbali zilizowasilishwa kwa madai kwamba hawazingatii kanuni.

Diwani wa Kata ya Mivinjeni, Frank Nyalusi (Chadema) alisema meya wao anaongoza vikao kibabe na kwa upendeleo na hivyo kuwanyima fursa wawakilishi hao wa wananchi kupata ufafanuzi wa mambo mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wananchi.

Nyalusi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadeama Jimbo la Iringa Mjini alisema watalazimika kumuita meya huyo kwenye vikao vyao vya chama (party  caucus) kwa ajili ya kumshauri ili atambue kwamba diwani sio mgonga muhuri wa mambo yanayoletwa katika vikao hivyo na watendaji wa halmashauri.

Diwani mwingine wa Chadema aliyepinga uendeshaji vikao wa meya huyo, Dadi Igogo wa kata ya Gangilonga alisema meya huyo anatakiwa kuendesha baraza hilo kwa kuzingatia kanuni na wala si kwa kuzingatia vyama au mahusiano yake na madiwani wengine.

“Leo ni lazima niseme ukweli, kiti cha meya kiliyumba, sijaridhishwa na namna kanuni zilivyokiukwa, na hasa kanuni namba 23; ni vizuri Meya awe anasoma kanuni ili asizitumie mahali pasipostahili kutumiwa kama anavyofanya yeye,” alisema.

Igogo alisema inashangaza kuona meya anawazuia madiwani kuuliza maswali ya nyongeza kutokana na majibu yasioridhisha ya maswali yao ya awali na jinsi anavyoonesha upendeleo kwa kuwaruhusu baadhi ya madiwani kuchangia hoja ambazo wengine wanazuiwa kufanya hivyo.

Naye Diwani wa Mshindo, Ibrahim Ngwada alisema uzoefu wao unaonesha kwamba tangu achaguliwe, meya huyo amekuwa akiingia katika vikao akiwa na ajande inayolenga kuwakamia baadhi ya madiwani.

Katika kikao cha jana, Ngwada alisema aliandika barua kuomba kuwasilisha hoja yake binafsi kwa mujibu wa kanuni ya 20, lakini azma yake hiyo ikapigwa chini kwa madai kwamba barua yake haikuainisha hoja anayotaka kuiwasilisha pamoja na kwamba kikanuni haimzuii kufanya hivyo.

Akizungumzia kilichotokea katika kikao hicho, mmoja wa wafuasi wa chama hicho, David Butinini alisema kwa kuwa baraza hilo ni jipya si jambo la ajabu endapo madiwani wake bila kujali vyama wanavyotoka wataonekana hawakubaliani kwa kuwa hiyo ndio demokrasia.

 “Lakini ni busara kutumia kikao cha chama cha madiwani, kukutana na kuelewana juu ya jambo wanalolizungumza kwenye baraza ili isitokee wakapingana wao kwa wao,” Butinini alisema.

Pamoja na kusisitiza kuliendesha baraza hilo kwa kuzingatia kanuni, Meya Kimbe ametetewa na baadhi ya madiwani wakisema kwamba wengi wao wanaona kama mambo hayaendi sawa katika vikao hivyo kwasababu hawajazijua vizuri kanuni za vikao hivyo.


Diwani wa Kata ya Mkwawa, Oscar Kafuka na wa kata ya Mkimbizi Severini Mtitu walisema baadhi ya madiwani wamekuwa wakitaka kuwasilisha hoja mahali ambapo hawatakiwi kufanya hivyo, na wanapozuiwa kwa kurudishwa kwenye kanuni, wanamlaumu meya.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment