Friday, 20 May 2016

KIJANA WA MIAKA 27 AUA MPENZI WAKE WA MIAKA 56 KWA WIVU


WATU wawili wamekufa mkoani Kagera kwa matukio mawili tofauti likiwamo mwanamke wa miaka 56 aliyeuawa na mpenziwe wa miaka 27 kwa kuchomwa kisu kifuani kwa wivu wa mapenzi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Augustine Ollomi, alisema tukio la kwanza lilitokea Mei 16 mwaka huu, saa nane usiku katika kijiji cha Lukole, kata ya Ihanda, wilayani Karagwe.

Alisema kijana aitwaye Eliudi Jonas (27) alikamatwa na Polisi baada ya kumuua mwanamke aliyetajwa kwa jina la Georgina Frances, (56) anayedaiwa kuwa mpenzi wake.

Akielezea tukio hilo, Kamanda Ollomi alisema wapenzi hao walikuwa na mfarakano ndipo Jonas aliinuka kitandani na kuchukua kisu na kumchoma Georgina kifuani hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na kupoteza maisha kabla ya kufikishwa hospitali.

Alisema baada ya mtuhumiwa huyo kufanya tukio hilo alitoroka na Mei 17 Polisi walifanya msako na kumkamata. Alisema upelelezi bado unaendelea na atafikishwa mahakamani muda wowote ukikamilika.

Katika tukio jingine, Kamanda alisema Mei 17 mwaka huu saa tano asubuhi katika kijiji cha Butembo, kata ya Buleza, wilayani Muleba mtu ambaye hajajulikana jina, anayekadiriwa kuwa na umri kati miaka 25 hadi 30, aliuawa na wananchi wasiojulikana.

Kamanda alisema watu hao walijichukulia sheria mkononi baada ya mtu huyo kuvamia na kuvunja nyumba saba kisha kuiba vitu mbalimbali wakati wenye nyumba hao wakiwa katika kazi za mashambani.

Alisema wananchi walimshambulia kwa mawe mtuhumiwa ambapo raia mwema alitoa taarifa Polisi Muleba na Polisi kabla hawajafika wananchi walikimbia. Polisi walimpeleka hospitali ya Wilaya lakini alifariki baada ya muda mfupi.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment