Saturday, 7 May 2016

Hili la Azam litubadilishe kufahamu kanuniLIGI Kuu Tanzania Bara inayoshirikisha timu 16 imebakiza mechi tatu kwa timu nyingi kufikia ukingoni.
Mbio za ubingwa hivi sasa zimebaki kwa wababe wawili, Yanga inayoongoza ikiwa na pointi 68 na Simba inayoshika nafasi ya pili ikiwa na pointi 58. Tofauti ya pointi kumi, ingawa Simba ipo nyuma mchezo mmoja.
Kimahesabu inaonekana Yanga tayari imeshakuwa bingwa kwani inahitaji pointi tatu tu kufikisha pointi 71, ambazo Simba haiwezi kuzifikia hata ikishinda mechi zake nne zilizosalia kwani itafikisha pointi 70.
Azam inashika nafasi ya tatu ikiwa na pointi 57 na ikishinda mechi zake tatu zilizosalia itafikisha pointi 66, hivyo ndio kusema imeshatolewa katika mbio hizo na kilichopo kwake ni kuwania nafasi ya pili.
Awali Azam ilikuwa katika mbio za ubingwa, lakini juzi Bodi la ya Ligi Kuu Tanzania Bara ilitangaza kuipoka Azam pointi tatu na mabao matatu ikidaiwa ilimchezesha beki Erasto Nyoni katika mchezo wao na Mbeya City akiwa na kadi tatu za njano kinyume cha kanuni.
Inasikitisha, lakini ni uamuzi ambao umetolewa kulingana na kanuni, hivyo kuiondoa Azam katika mbio hizo na kuacha wababe Simba na Yanga wakiumana wenyewe. Hatutaki kujadili kuhusu hilo, lakini tunasema inaeleweka kwamba mashindano yoyote yale ili yaendeshwe kwa ufanisi na ushindani wa haki ni lazima yawe na kanuni.
Na si tu kuwa na kanuni, bali pia ziwe zinaeleweka kwa wahusika. Kama ilivyo kwa Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) nalo linaendesha mashindano yake kwa kutumia kanuni. Ili timu iwe mshiriki na mshindani wa kweli katika michuano hiyo ni lazima iwe na ufahamu katika michuano husika.
Ni rahisi timu kupoteza ushindi, kupigwa faini na hata kupokwa haki ikiwa haina ufahamu wa kanuni. Kama timu inashiriki mashindano halafu haifahamu kanuni za mashindano husika inawezaje kuwa mshindani wa kweli?
Ni kawaida kwa klabu za Tanzania katika ngazi mbalimbali, hata mashindano ya kugombea mbuzi kuingiza timu bila kuomba, kupewa au kutaka kufahamu kanuni kwa mashindano husika. Hali hiyo husababisha vurugu katika mashindano kwa vile timu inaposhindwa mechi hulalamikia vitu vingine ambavyo kwa mujibu wa kanuni havikupaswa kulalamikiwa, lakini kwa upofu wa kanuni timu au klabu hulalamika.
Hufika mahali klabu inaelekeza nguvu katika malalamiko au rufani kuliko kuwekeza katika timu ili iweze kufanya vizuri, ambapo matokeo yake ni kutokuwepo ushindani kutoka kwa timu husika au mashindano yenyewe kwa ujumla. Kanuni ndiyo mwongozo wa kila kitu katika mashindano.
Timu ikitaka iharibikiwe katika mashindano iache kuzingatia kanuni na mfano wa hili tumeuona kwa Azam. Pia ikumbukwe kuwa kanuni zote katika mashindano ni sawa. Dhana kuwa kanuni hii ndiyo mama na ya msingi si sahihi hata kidogo, kwa vile kanuni zote zimewekwa au kutengenezwa kwa sababu maalumu.
Klabu inayowajibika ni ile inayozingatia kanuni badala ya kufanya mambo kwa kubahatisha kwa dhana kuwa wasimamizi wa mashindano au klabu pinzani haiwezi kubaini ukiukwaji wa kanuni husika.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment