Friday, 22 April 2016

Yanga sasa na Waangola CAF

Kikosi cha Sagrada Esperanca ya Angola
SIKU moja baada ya kutolewa na Al Ahly ya Misri katika hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Yanga imeangukia kwa Sagrada Esperanca ya Angola katika michuano ya kuwania ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Itakutana na Waangola hao katika hatua ya mtoano ambayo mshindi wake ataingia hatua ya makundi ya michuano hiyo inayoshika nafasi ya pili kwa ukubwa katika ngazi za klabu barani Afrika.
Kwa mujibu wa ratiba iliyopangwa na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) jana alasiri, Yanga baada ya kufungwa 2-1 na Ahly juzi usiku huko Alexandria na hivyo kutolewa kwa jumla ya mabao 3-2, sasa itakipiga dhidi ya timu hiyo inayomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa la Angola.
Itaanza kwa kuwakaribisha Waangola hao kati ya Mei 6 na 8 jijini Dar es Salaam na marudiano kuwa kati ya Mei 17 na 18 nchini Angola.
Haijafahamika Angola zitachuana katika mji gani, ingawa Sagrada iliyoanzishwa Desemba 22, mwaka 1976, yaani miaka 39 iliyopita, uwanja wake wa nyumbani upo Dundo, katika Jimbo la Lund Norte ambao una uwezo wa kuingiza mashabiki 3,000 kwa wakati mmoja.
Endapo itafanikiwa kuwang’oa Sagrada inayonolewa na Zoran Mackic, raia wa Serbia, Yanga itakuwa imejihakikishia kusaka mamilioni ya fedha katika michuano hiyo ambayo mshindi wake hutwaa kitita cha dola za Kimarekani 625,000 (Sh bilioni 1.36).
Mshindi wa pili hupata dola 432,000 (Sh milioni 907) wakati timu zinazoshika nafasi ya pili na ya tatu katika kila kundi hupata dola 239,000 (Sh milioni 500) na ya mwisho katika kundi, yaani inayoshika nafasi ya nne, huambulia dola 150,000 (Sh milioni 315).
Wakati Yanga ikiangukia kwa Waangola, waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, TP Mazembe waliovuliwa ubingwa juzi, watakutana na Waarabu wa Tunisia, Stade Gabesien, huku Esperance pia ya Tunisia iliyoitoa Azam FC ikipangwa kukutana na Mo Bejaiaa ya Algeria.
Michezo mingine ya mtoano itakuwa kati ya Stade Malien (Mali) na FUS Rabat (Morocco), Etoile du Sahel (Tunisia) na CF Mounana (Gabon), Al-Ahli Tripoli (Libya) na Misr El-Makasa (Misri), Al-Merreikh (Sudan) na Kawkab Marrakech (Morocco), wakati Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini itacheza na Medeama ya Ghana.
Yanga na timu nyingine zilizotolewa katika Hatua ya 16 Bora ya Ligi ya Mabingwa Afrika, zimeangukia Kombe la Shirikisho kama Kanuni za CAF zinavyoeleza kuwa, timu ambazo zitatolewa katika Raundi ya Pili ya Ligi ya Mabingwa zitaangukia Kombe la Shirikisho kukutana na timu nane zilizosonga mbele ambapo zitacheza mechi za mtoano za nyumbani na ugenini kisha zitakazofuzu zitaingia hatua ya makundi.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment