Wednesday, 27 April 2016

WANAOTAKIWA KUPISHA UJENZI WA BARABARA MJINI IRINGA WAANDAMANA KUDAI FIDIA


BAADHI ya wananchi wenye nyumba zinatakiwa kubomolewa mjini Iringa ili kupisha ujenzi wa mradi wa barabara ya mchepuko inayounganisha barabara kuu mbili, wameandamana hadi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza wakiishinikiza serikali kuwalipa fidia.

Wananchi hao walijenga na kuwekeza katika eneo hilo lililopo jirani na Chuo Kikuu cha Iringa (IUCO), kata ya Kihesa mjini hapa ambako serikali imeona panafaa kupitisha barabara hiyo itakayounganisha barabara kuu ya Iringa Dodoma na ile inayounganisha barabara ya Iringa, Dar es Salaam na Mbeya.

Kwa zaidi ya miaka mitano Kikao cha Ushauri cha Mkoa wa Iringa (RCC) kimekuwa kikiomba serikali itoe fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ili isadie kupunguza msongamano wa magari, hasa makubwa yanayopita katikati ya mji wa Iringa yakitokea na kuelekea Mbeya na Dodoma.

Mwenyekiti wa umoja wa waathirika hao, Stanford Mwakasala alisema baada ya kutaarifiwa juu ya maamuzi hayo ya serikali, mwaka 2012, mali na nyumba zao vilifanyiwa uthamini kwa lengo la kupewa fidia.

“Baada ya uthamini huo, tulizuiwa kufanya maendelezo yoyote ya mali na nyumba zetu katika eneo hilo,” Mwakasala alisema.

Alisema pamoja na zuio hilo, hakuna mwathirika yotote aliyelipwa fidia yake na hali ya nyumba na mali zingine zilizopo katika maeneo yao zinaendelea kuharibika.

“Tumeandamana hadi hapa ofisini kwa Mkuu wa Mkoa baada ya kuona hakuna dalili za kulipwa fidia zetu, tuliandika barua kwa waziri wa Ujenzi,Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa lakini hatujapata ushirikiano wowote, tunataka Mkuu wa Mkoa asikie kilio chetu ,”alisema .

Naye Herieth Magambo alisema kitendo cha kuchelewa kulipwa fidia kimewarudisha nyuma kimaendeleo kutokana na nyumba zao kutowaingizia kipato kwa kipindi cha miaka minne.

“Nyumba zetu zimekosa wapangaji kwani wanaogopa kuingia na kuishi kwenye nyumba ambazo wanajua wakati wowote zitabomolewa na kwa kuzingatia kwamba wengi wetu tulijua ujenzi wa barabara hiyo utafanyika wakati barabara ya Iringa Dodoma ukiendelea,” alisema.

Alisema baadhi ya nyumba zenye wapangaji, zimeendelea kutumika bila kufanyiwa ukarabati kwa hofu ya kupata hasara kwa kuzingatia agizo lenyewe la serikali linalozuia ukarabati au uendelezaji wa mali na nyumba hizo.

Akizungumza na wananchi hao Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Masenza alisema; “Nimesikia kilio chenu na hata mimi nilikuwa  nalia pamoja nanyi, ninawahakikishia kuwa serikali itawalipa fidia zenu, naomba muendelee kuvuta subira.”


Masenza alisema ukosefu wa fedha serikalini ulisababisha wananchi hao wachelewe kulipwa fidia zao lakini akawahakikishia kuwepo kwa mpango huo katika bajeti ya mwaka ujao wa fedha, 2016/2017.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment