Thursday, 28 April 2016

TCCIA YAWAIKUTANISHA SEKTA BINAFSI NA YA UMMA KATIKA MEZA YA MAJADILIANOCHEMBA ya Biashara, Viwanda na Kilimo (TCCIA) Mkoa wa Iringa imesema uamuzi wa serikali ya Rais Dk John Magufuli wa kufunga akaunti za mashirika na taasisi zake katika mabenki ya biashara na kuhamishia fedha zake Benki Kuu (BoT) utasaidia kuikuza sekta binafsi nchini.

Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Iringa, Lucas Mwakabungu aliyasema hayo jana kwenye warsha ya mafunzo ya dawati la majadiliano kati ya sekta ya umma na binafsi, iliyofanyika kwa siku mbili katika ukumbi wa Gentle Hills, mjini Iringa.

“Uamuzi huo wa Mheshimiwa Rais wetu mpendwa utasaidia sana kushusha riba za mabenki yetu ya biashara kwasababu sekta binafsi ndiyo itakayokuwa mteja mkubwa wa mabenki hayo,” alisema.

Pamoja na kuipongeza serikali kwa kazi kubwa inayofanya ya kuboresha mazingira yanayokuza sekta binafsi, Mwakabungu alisema bado mazingira ya biashara yameendelea kuwa katika changamoto nyingi.

Alizitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni pamoja na kodi nyingi, masoko ya bidhaa na huduma kutokuwa ya uhakika, miundombinu mibovu ya barabara na ukosefu wa umeme vijijini, matumizi ya pembejeo feki na sheria ya vipimo na mizani kutosimamiwa ipasavyo.

Nyingine zinahusu wakulima kuuza mazao yao kwa bei ya chini ya gharama za uzalishaji kwasababu ya ukosefu wa bei elekezi, ukubwa wa ushuru wa mazao na ulipiaji wa leseni za biashara ambao ni kikwazo kikubwa katika urasimishaji wa biashara.

Kwa kupitia warsha hiyo ambayo mbali na kushirikisha wawakilishi toka sekta binafsi, iliwashirikisha pia wakuu wa wilaya, wakurugenzi na wenyeviti wa halmashauri za mkoa wa Iringa, Mwakabungu alisema wadau hao wamepata stadi juu ya umuhimu wa majadiliano kati ya sekta binafsi na ya umma ili kuharakisha maendeleo.

“Lakini warsha hii imetusaidia kujenga imani ya pamoja kati ya sekta hizi mbili katika utatuaji wa kero za maendeleo ya uchumi wetu katika mkoa wa Iringa na taifa kwa ujumla,” alisema.

Akifungua warsha hiyo iliyofadhiliwa na Best Dialogue, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza alisema ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi ndio utakaoihakikishia nchi maendeleo.

“Maeneo ambayo TCCIA inayafanyia kazi yaani biashara, viwanda na kilimo ndio njia kuu za uchumi wa nchi, kwahiyo meza ya majadiliano baina ya sekta hizo ndio inayoweza kuharakisha maendeleo yake,” alisema.

Alisema sekta ya umma na binafsi zinapaswa pia kushirikisha watafiti ili kuondosha changamoto ambazo ni kero katika ukuaji wa sekta binafsi.

“Naomba TCCIA kwa kushirikiana na Best Dialogue waangalie pia uwezekano wa kutoa mafunzo hayo ya meza ya pamoja kwa ngazi ya wakuu wa idara zote za halmashauri na madiwani wake ili wawe katika mkakati wa kuboresha mazingira hayo,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment