Thursday, 7 April 2016

TANAPA, UNDP WASAIDIA WAATHIRIKA WA MAFURIKO IRINGASHIRIKA la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) wametoa msaada wa bati 509 na mifuko 505 ya saruji kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa nyumba za kudumu za kaya 100 ambazo hivi karibuni zilikumbwa na mafuriko katika tarafa ya Pawaga wilayani Iringa, mkoani Iringa.

Akikabdhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, Dk Christopher Timbuka alisema una thamani ya zaidi ya Sh Milioni 14.95.

Dk Timbuka alisema wakuu wa taasisi hizo mbili waliguswa na mafuriko yaliyoziathiri kaya hizo na kuamua kuchangia vifaa hivyo vya ujenzi kwa kuzingatia pia kwamba tarafa ya Idodi na Pawaga ni wadau muhimu wa uhifadhi kwa kuwa wanapakana na hifadhi ya taifa ya Ruaha.

Mwakilishi wa UNDP, Gertrude Lyatuu na Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Maeneo yaliyohifadhiwa Kusini mwa Tanzania (SPANEST), Godwel Olle Meing’ataki walisema wakisaidiwa, waathirika hao watakuwa katika nafasi nzuri ya kushirikiana na wadau wengine kutekeleza mikakati ya kupambana na ujangili.

Akishukuru kwa msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema; “misaada yote inayotolewa kwa ajili ya wathirika hao itatumika kwa lengo lilikusudiwa na si vinginevyo kwahiyo nawaomba mtusaidie kutufikishia msaada wenu huu kijijini kwa walengwa.”

Alisema waathirika hao walipewa viwanja katika kijiji cha Kisanga, Pawaga ambako watajenga nyumba bora tofauti na zile walizokuwa wakiishi awali ambazo nyingi kati yake zilikuwa za tope.

“Tunaendelea kufyatua tofali, kazi inayosimamiwa na Mkuu wa Wilaya ya Iringa Richard Kasesela; wiki ijayo tutakwenda huko ili kujionea hatua iliyofikiwa na ni matumaini yetu ujenzi wa nyumba hizo utaanza wakati wowote baada ya hapo,” Masenza alisema huku akisistiza kwamba pamoja na misada hiyo bado mahitaji ya bati ni makubwa.

Akizungumzia mkakati wa ujenzi wa nyumba bora kwa ajili ya wathirika hao, Mkuu wa Wilaya ya Iringa alisema tofali zinazoendelea kufyatuliwa zaitagaiwa kwa walengwa ili wazitumie kujenga nyumba zao katika viwanja walivyopimiwa.

Alisema tathimini yao ya awali inaonesha kila kaya itapata wastani wa tofali 1500 watakazozitumia kujenga nyumba yenye vyumba viwili, sebule na choo.

“Hiyo haina maana waathirika hao hawaruhusiwi kujenga nyumba kubwa zaidi ya zinazopendekezwa, ruksa hiyo wanayo lakini watakachotakiwa kufanya ni kutumia nguvu zao kuongeza pale msaada wa serikali na wadau wake utakapoishia,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment