Friday, 1 April 2016

SERIKALI KUPITIA UPYA MIKATABA YA UNUNUZI WA MABEHEWA NA VICHWA VYA TRENI


Serikali imeliagiza Shirika la Reli Tanzania (TRL), kupitia upya mikataba ya ununuzi wa vichwa vya treni na mabehewa ili kubaini kasoro zilizojitokeza na kuchukua hatua stahiki kabla ya maboresho ya reli ya Tanga-Moshi-Arusha.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametoa agizo hilo mkoani Kigoma wakati akikagua miundombinu ya reli na kusisitiza nia ya serikali ya kufufua reli ya kanda ya kaskazini ili kuimarisha huduma ya uchukuzi katika mikoa ya Tanga, Kilimanjaro na Arusha.

“Kama Serikali tumewekeza vya kutosha katika TRL, hivyo tunawataka mfanye biashara itakayolipa nasi tutahakikisha popote reli ilipo inatoa huduma iliyokusudiwa na kuchangia kukuza uchumi wa nchi,” amesema Prof. Mbarawa.

Amesema Serikali imedhamiria kuliongezea nguvu TRL ambapo baadhi ya mitambo kutoka Kampuni Hodhi ya Rasilimali za Reli (RAHCO) itakabidhiwa kwa shirika hilo hivyo kulitaka kuwa na mpango madhubuti wa kufanya biashara na kurudisha hadhi ya usafiri wa reli hapa nchini.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment