Friday, 1 April 2016

RICHARD NDASSA ABURUZWA MAHAKAMANI AKITUHUMIWA KUOMBA RUSHWA


Mbunge mwingine wa Jimbo la Sumve, Richard Ndassa (CCM) amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu leo akituhumiwa kuomba rushwa ya shilingi milioni 30 akiwa kwenye Kamati za Bunge.

Ndassa anakuwa mbunge wanne kutoka CCM kufikishwa kizimbani hapo baada ya wabunge watatu, Mbunge wa Mvomero, Ahmad Saddiq (53), Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (54) na wa Lupa, Victor Mwambalaswa (63) kufikishwa jana katika mahakama hiyo wakituhumiwa kwa tuhuma hizohizo.

Akisomewa mashtaka dhidi yake mbele ya Hakimu Mkazi Emilius Mchauru,Ndassa anadaiwa kiwa kama mjumbe wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji March 13, mwaka huu alimwomba rushwa ya shilingi Milioni 30 kutoka kwa Mtendaji Mkuu wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) Bw. Felchesmi J. Mramba ili amsaidie kuwashawishi wajumbe wengine wa Kamati ya Mtaji na Uwekezaji kupitisha bila kipingamizi taarifa ya TANESCO kwa mwaka 2015/2016.

Mshtakiwa yupo nje kwa dhamana baada ya kupata mdhamini mmoja na kulipa shilingi milioni 10. Uchunguzi wa shauri hili bado unaendelea na kesi hii itatajwa tena tarehe 18/4/2016.

Kwa wabunge waliofikishwa jana inadaiwa mnamo Machi 15 mwaka huu, kati ya saa mbili na saa nne usiku katika Hoteli ya Golden Tulip, Kinondoni, Dar es Salaam, kwa pamoja wakiwa kama wabunge na wajumbe wa Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa, waliomba na kushawishi kupewa rushwa ya Sh milioni 30 kutoka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Gairo, Mbwana Magotta.

Wabunge hao waliomba kiasi hicho cha pesa, kama kishawishi cha kutoa mapendekezo ya hati safi kwa halmashauri hiyo, jambo ambalo ni kinyume cha sheria. Baada ya kusomewa mashitaka, washitakiwa walikana kutenda kosa hilo na upande wa Jamhuri ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo, unaendelea na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment