Wednesday, 13 April 2016

MKATABA WA JESHI LA POLISI NA LUGUMI ENTERPRISES KITENDAWILI


JESHI la polisi limeshindwa kuwasilisha mkataba wake na kampuni ya Kampuni Lugumi Enterprises iliyotakiwa kufunga mashine za alama za vidole kwenye vituo vya polisi, kama walivyoagizwa na kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma (PAC).

Wiki iliyopita, PAC ilitoa siku sita kwa jeshi hilo wawe wamewasilisha nyaraka za mkataba huo wenye thamani ya Sh bilioni 37.

“Jana (juzi) ilikuwa siku ya mwisho kwa jeshi kuwasilisha mkataba huo ofisi za Bunge, lakini mpaka leo (jana) muda huu ninapozungumza nanyi (saa 7:30 mchana) walikuwa hawajawasilisha,” alisema Mwenyekiti wa Kamati ya PAC, Aeshi Hilaly.

Alisema kamati hiyo imetoa siku tatu tangu barua itakapopelekwa na ofisi za Bunge, kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kamati hiyo iweze kupitia utekelezaji wa mkataba huo na baadaye kupeleka mapendekezo kwenye Bunge.

Kamati ya PAC ilipokuwa ikipitia hesabu za Jeshi la Polisi, ilibaini kuwapo mkataba tata wa Kampuni ya Lugumi wa mwaka 2011, ambapo kampuni hiyo ilipewa zabuni ya kufunga mashine za kuchukua alama za vidole katika vituo vya polisi 108 nchini kwa gharama ya Sh bilioni 37.

Inasadikiwa kampuni hiyo imekwishalipwa Sh bilioni 34 kati ya Sh bilioni 37, huku ikiwa imefunga mashine katika vituo 14 pekee katika jiji la Dar es Salaam, ambavyo pia inadaiwa havijulikani maeneo vilipo.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment