Monday, 4 April 2016

MFAMASIA WA HOSPITALI YA MKOA WA IRINGA NA WILAYA YA MUFINDI WANASWA NA TAKUKURU


WAFAMASIA wawili, mmoja wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na mwingine wa hospitali ya wilaya ya Mufindi pamoja na watuhumiwa wengine wawili waliokuwa viongozi wa kijiji cha Ilula Mwaya wilayani Kilolo wamefikishwa mahakamani kati ya Januari na Machi mwaka huu wakituhumia kwa makosa mbalimbali ya rushwa.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi ya kipindi hicho, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa, Eunice Mmari alisema watuhumiwa hao wanne wamefikishwa mahakamani kwa mujibu wa Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Namba 11 ya mwaka 2007.

Aliwataja wafamasia hao kuwa ni Lucas Mwandi wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Iringa na Selemani Fulano wa hospitali ya wilaya ya Mufindi, na Deogratias Vangiliasas aliyekuwa Mwenyekiti wa kijiji cha Ilula Mwaya na Robert Kisaka aliyekuwa afisa mtendaji wa kijijiji hicho.

Azungumza na wanahabari ofisini kwake jana, Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Iringa, Eunice Mmari alisema wafamasia hao wanashitakiwa kupitia kesi namba 53/2016 na kesi namba 39/2016 kwa makosa ya wizi wa mali ya umma wakiwa mtumishi wa umma kinyume na kifungu cha 270 cha sheria ya kanuni ya adhabu iliyorekebishwa mwaka 2002.

Kuhusu waliokuwa viongozi wa kijiji hicho, alisema nao wanashitakiwa kwa makosa ya wizi wa mali za umma kupitia kesi namba 23/2016, kinyume na sheria hiyo ya rushwa kifungu namba 28, 29, 30 na 31.

Mmari alisema katika kipindi hicho cha Januari hadi Machi, Takukuru pia imepokea malalamiko 28 ya rushwa na 14 kati yake yamefunguliwa majadala ya uchunguzi, malalamiko tisa yanafanyiwa uchunguzi wa awali, huku malalamiko matano yakifungwa baada ya kukosekana kwa ushahidi.

Alikitoa mchanganuo wa mamalamiko hayo alisema afya iliongoza kwa kuwa na malalamiko saba, serikali za mitaa, vijiji na kata (6), elimu (3), ardhi (2), sekta binafsi (1), Tanroads (1), Ushirika na Kilimo (2), Polisi (1), Ujenzi (1) na sekta binafsi (2).

Akizungumzia mwamko wa wakazi wa mkoa wa Iringa kuyaripoti matukio ya rushwa katika taasisi yao, Mmari alisema; “mwamko ni mdogo sana ikilinganishwa na mikoa mingine.”

Alisema Takukuru inaamini kuwepo kwa makosa mengi yanayoangukia katika sheria ya rushwa lakini yemekuwa hayaripotiwi katika taasisi yao jambo linalowaathiri wananchi wenyewe na uchumi wa Taifa.

Aliwataka wananchi hao kutoa taarifa kwao wakati wowote wanapokosa huduma baada ya kudaiwa rushwa au pale wanapobaini miradi ya maendeleo katika maeneo yanayowazunguka inafanywa chini ya kiwango.

Kwa kupitia elimu kwa umma, Mmari alisema wananchi 4,957 wamepatiwa elimu ya rushwa katika kipindi hicho, wakiwemo wanafunzi 3,693.

Alisema ofisi yao pia imefanya vikao vinne vya kujadili dhibiti zilizofanyika ili kuziba mianya ya rushwa katika usimamizi wa mali za vijiji, zabuni ya ununuzi wa pampu ya kusukuma maji katika mji wa Mafinga, ajira za vibarua katika mamlaka ya maji Mafinga na taratibu za kuchukua walimu wa kujitolea shule za msingi za mjini Iringa.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment