Wednesday, 27 April 2016

MAKATIBU TAWALA WA MIKOA WAPYA WAAPISHWA, WAHIMIZWA KUPAMBANA NA RUSHWA


Rais Dk John Magufuli amewaapisha Makatibu Tawala kumi (10) wapya ambao aliwateua mwanzoni mwa wiki hii na kuwapangia vituo vya kazi.

Baada ya kuapishwa, makatibu tawala hao wametia saini hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, zoezi lililoendeshwa na Kamishna wa maadili Sekreatieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mheshimiwa Jaji Salome Kaganda na kushuhudiwa na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi.

Akizungumza baada ya kusaini ahadi ya uadilifu, Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi amewaasa makatibu tawala hao kufanya kazi kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya na mikoa na kuhakikisha rushwa inatoweka katika ngazi zote.

“Wasimamieni walio chini yenu ili haya maadili mliyoyasaini leo yaweze kusambaa kwa watumishi wote,” alisema balozi Kijazi.


Makatibu Tawala wengine wa Mikoa ambao hawakuapishwa leo, ni wale waliohamishwa vituo vya kazi na wale waliobaki katika vituo vya kazi walivyokuwepo ambao tayari walishakula kiapo cha kuwa Katibu Tawala wa Mkoa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment