Monday, 11 April 2016

MADEREVA WA MASAFA MAREFU WAJENGEWA VITUO VYA USHAURI NA UPIMAJI AFYA BARABARANI

MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza amezindua vituo viwili vya huduma za afya  na upimaji virusi vya Ukimwi (VVU) kwa hiari vilivyojengwa kandokando ya barabara kuu ya Iringa Dar es Salaam, mkoani Iringa vikilenga kutoa huduma hizo kwa madereva wa masafa marefu.

Vituo hivyo ambavyo pia vitatoa huduma kwa wananchi wanaovizunguka, vimejengwa katika mji mdogo wa Ilula, wilayani Kilolo na kijiji cha Wenda, Iringa Vijijini kwa msaada wa wadau wa sekta ya usafirishaji nchini watakaogharamia uendeshaji wake hadi mwaka 2018.

Meneja wa kampuni ya Impala Terminals Tanzania ambayo ni sehemu ya wadau hao, Jorge Rico Grillo alisema kampuni yao kwa kushirikiana na mashirika ya  Puma Energy Foundation na Trafigura walitoa fedha kwa shirika la kimataifa linalojishughulisha na afya la North Star Alliance na kujenga vituo hivyo.

Grillo alisema pamoja na vituo hivyo viwili, wadau hao wamejenga vituo vingine vinne katika mikoa ya Dar es Salaam na Mbeya vilivyozinduliwa kwa nyakati tofauti wiki iliyopita.

Alisema lengo lao ni kuona madereva wanaotumia barabara hiyo inayokwenda hadi nchi za Malawi na Zambia wanakuwa katika mazingira rafiki yatakayowawezesha kupata ushauri na huduma mbalimbali za afya wakiwa safarini.

Mwakilishi wa shirika la North Star Alliance, John Mwachama alisema kwa kupitia vituo hivyo madereva watapata elimu ya afya, madhara ya dawa za kulevya na pombe pamoja na huduma bure ya upimaji na matibabu wa magonjwa mbalimbali ikiwemo VVU, kisukari na mengineyo jambo litakalowawezesha kuchukua tahadhari kabla na wakati wakitumia barabara hiyo.

Meneja Uendeshaji wa Puma Energy Tanzania, Lameck Hiliyai alisema kujengwa kwa vituo hivyo kutasaidia makampuni ya usafirishaji kuwatumia madereva wanaojali afya zao.

Mwakilishi wa kampuni za usafirishaji, Arif Abri wa kampuni ya FM Transporter alisema hakuna udereva salama kama madereva hawatakuwa na tabia ya kujua hali za afya zao.

Abri alisema dereva akijua afya yake itamuwezesha kufanya maamuzi ya busara yanayoweza kusaidia mikakati mbalimbali ya serikali ya kupunguza hasara na vifo vinavyotokana na ajali.

Akizindua vituo hivyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alisema vituo hivyo vitakuwa vya manufaa sana kwa madereva na wananchi walio jirani navyo kwani vinaongeza upatikanaji wa huduma zinazotolewa pia katika vituo vingine binafsi na vya serikali.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment