Monday, 11 April 2016

LUPIMO SANITARIUM CLINIC YATOA MSAADA WA MADAWATI IRINGA


SHULE ya Msingi Ipogolo ya mjini Iringa imepata msaada wa madawati 50 yenye thamani ya zaidi ya Sh Milioni 3 yaliyotolewa na kituo cha tiba asilia na tiba mbadala cha Lupimo Sanitarium Clinic chenye tawi lake mjini hapa.

Mkuu wa shule hiyo yenye changamoto lukuki, Amani Mkeremy alisema watoto wengi wa shule hiyo yenye wanafunzi 1,328 wanakaa chini kwa kuwa tatizo la madawati ni kubwa linalohitaji kutatuliwa kwa misaada ya wadau mbalimbali wa sekta ya elimu.

Akishukuru kwa msaada huo aliosema utsaidia kupunguza tatizo hilo, Mkeremy alisema wakati mahitaji ya shule ni madawati 664, yaliyopo ni 300 tu jambo linalofanya mazingira ya kufundishia wanafunzi hao shuleni hapo yawe magumu.

Akikabidhi msaada huo kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa Amina Masenza juzi, Mkurugenzi wa Lupimo Sanitarium Clinic Dk John Lupimo alisema; “tumemtoa msaada huu ikiwa ni mkakati wetu wa kurudisha kwa jamii sehemu ya kile tunachopata kutoka kwao.”

Lupimo alisema mpango wa serikali ya Dk John Magufuli wa kutoa elimu bure kwa wanafunzi wa shule za msingi hadi sekondari utakuwa wa mafanikio makubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu endapo wadau wake watashiriki kuzimaliza changamoto mbalimbali zinazoikabili.

Akipokea msaada huo kwa niaba ya shule hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Iringa alishtushwa kusikia shule hiyo mbali na kuwa na upungufu mkubwa wa madawati lakini pia ina upungufu wa vyumba 18 vya madarasa na matundu 28 ya choo.

Alipokuwa akiwasilisha taarifa yake kwa mkuu wa mkoa, mkuu wa shule hiyo alisema; “ shule hii iliyoanzishwa mwaka 1972 ina vyumba vya madarasa 18 tu wakati mahitaji ni vyumba 35 na ina matundu ya vyoo 32 wakati mahitaji ni matundu 60 kwa ajili ya wavulana na wasichana.”

Akioneshwa kukerwa na taarifa hiyo inayodhihirisha wanafunzi hao kusoma katika mazingira magumu, Mkuu wa Mkoa Masenza alisema atalazimika kumfuta kazi afisa mtendaji wa kata ya Ipogolo (Ruaha),Bahati Mlafi endapo itabainika katika mpango wake wa maendeleo hakuna mkakati wa kumaliza tatizo hilo.

Akijitetea Mlafi alisema wabao mpango wa kuboresha mazingira ya shule hiyo yanayohusisha kuihamisha kutoka katika eneo ilipo kwasababu ya udogo wake ili wapate eneo kubwa litakalokidhi mahitaji.

Akimshukuru Dk Lupimo kwa msaada huo alisema; “lazima kila shule iwe na sheria itakayowalazimisha wazazi kulipa madawati yanayoharibiwa kwa makusudi na wanafunzi.”

Akizungumzia upungufu wa madawati mjini Iringa, Masenza alisema kuna upungufu wa madawati 3000 kwa shule za msingi na 334 kwa shule za sekondari.


Awali Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema; “Changamoto ya madawati katika shule mbalimbali za wilaya hiyo ni kubwa lakini pamoja na ukubwa wake tunapambana nayo ili kabla ya April 30 kila shule iwe na madawati yanayohitajika.”

Reactions:

0 comments:

Post a Comment