Wednesday, 13 April 2016

KIKWETE AFURAHI MAISHA YA URAIANI


MIEZI mitano tangu atoke madarakani, Rais wa awamu ya nne, Dk Jakaya Kikwete amesema kwa sasa anafurahia maisha ya uraiani na kwamba anajiandaa kuwa mzee mashuhuri nchini atakapokabidhi chama.

Akihojiwa na Idhaa ya Kiswahili ya BBC, Kikwete alisema maisha nje ya Ikulu ya Magogoni ni mazuri kwa sababu ametua mzigo wa kuhudumia watu milioni 50 na kwamba sasa anaendelea na mambo yake binafsi.

“Maisha baada ya kutoka madarakani ni mazuri kwa sababu sina presha niliyokuwa nayo, nilikuwa na mzigo mkubwa wa kuangalia taifa hili la watu milioni 50, siyo mzigo mdogo, ni kazi kubwa… Sasa hivi unarudi nyumbani hauna faili, ninafanya mambo ninayoyapanga mimi, na shughuli ninazofanya ni za kimataifa tu, niko kwenye hili la Libya (mjumbe wa usuluhishi wa mgogoro wa Libya), naondoka karibuni, tuna mkutano Marekani wa mambo ya malaria,” Kikwete aliiambia BBC.

Mbali na shughuli hizo, kwa sasa Kikwete yupo kwenye Kamisheni ya Elimu na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Gordon Brown na pia ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

“Kuhusu siasa, bado ni Mwenyekiti wa CCM na baada ya muda, nitakabidhi baada ya hapo kila kitu nitamuachia mzee Magufuli aendelee nayo, mimi nitabaki ni mzee tu maarufu katika nchi yetu, maisha ni mazuri tu,” alisema Kikwete.

Tangu alipoachia kiti cha urais na kumkabidhi Dk. John Magufuli baada ya kuapishwa Novemba 5, mwaka jana, Kikwete amekuwa akiishi nyumbani kwake Msoga mkoani Pwani baada ya kuhamia huko na familia yake, Novemba 6, mwaka jana.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment