Friday, 1 April 2016

FEDHA ZA TASAF KILOLO KUWATOKEA PUANI WANAOZITUMIA KWA ULEVI

HALMASHAURI ya wilaya ya Kilolo imezinyoshea kidole kaya zinazonuifaka na Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini ikiahidi kuziondoa zile zinazotumia kwa ulevi na matumizi mengineyo yasiyokubalika, fedha wanazopewa kwa ajili kugharamia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na maji.

Jumla ya kaya masikini 6,464 za halmashauri hiyo zinanufaika na fedha za mpango huo zinazotolewa kila baada ya miezi miwili kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF).

Mratibu wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini Kilolo, Venance Mwaikambo alisema; “halmashauri yetu ilianza kunufaika na mpango huo toka Julai mwaka jana na hadi mwezi Machi mwaka huu kaya hizo zilikuwa zimepata malipo ya tano ya zaidi ya Sh Milioni 198 kwa ajili ya mwezi Machi na April.”

Wakati kaya hizo zikijipatia kati ya Sh 20,000 na Sh 70,000 kila baada ya miezi miwili, Mwaikambo alisema zipo taarifa zinazoendelea kuchunguzwa zikihusisha baadhi yao kuzitumia fedha hizo kununua pombe na matumizi ya starehe na michango isiyo ya lazima.

“Serikali haijaleta fedha hizi kama zawadi, inataka ziwatoe kutoka hatua moja hadi nyingine,” alisema huku baadhi ya kaya zikikiri kuanzisha miradi midogo midogo ya ufugaji na kilimo, kuwapeleka na kuwanunua watoto mahitaji ya shule na kugharamia huduma za afya.

Mwaikambo alisema serikali haiwezi kukubali kuendelea kutoa fedha kwa watu wanaozitumia kwa pombe na wamekwishapeleka maombi TASAF ya kuwaondoa na kuziingiza kwenye mpango kaya nyingine mpya.

Afisa ushauri na ufuatiliaji wa mpango huo wa TASAF wilayani Kilolo, Happy Mpuya alisema serikali kwa kupitia mpango huo inatoa ruzuku ya msingi na ya masharti nafuu kwa kaya masikini ili kugharamia mahitaji ya msingi ikiwemo elimu, afya na maji.

Mpuya alisema ruzuku ya msingi inatolewa kwa kila kaya iliyoandiskishwa kwenye mpango ili kugharamia mahitaji hayo ya msingi na ruzuku ya masharti nafuu inatolewa kwa kaya masikini zenye watoto wenye umri wa kwenda shule na kliniki.

“Msije mkashangaa fedha mnazopata zinapungua kwasababu ya mahudhurio hafifu ya watoto wenu shuleni na wale ambao wanatakiwa kupelekwa kliniki hawapelekwi. Nataka mjue tuna utaratibu wa kufuatilia taarifa zenu za jinsi fedha hizo zinavyowanufaisha,” alisema.


Alisema kaya zitakazobainika kuzitumia fedha hizo kinyume na malengo hayo zitaondolewa katika mpango kama masharti ya mpango yanavyotaka fedha hizo zisitumike kwa shughuli nyingine tofauti na za mpango.

Mmoja wa wanufaika wa mpango huo, Upendo Geufeni wa kijiji cha Itunda aliyepata jumla ya Sh 100,000 toka Julai mwaka jana alisema; “fedha hizo zinamsaidia kwa matibabu na akiba ndogo anayojiwekea imemuwezesha kufuga kuku.” alisema.

Dada huyo mlemavu aliiomba serikali kuboresha mpango huo kwa kutoa msaada utakaowawezesha kujenga nyumba bora.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment