Monday, 4 April 2016

CUF YATANGAZA KUTOMTAMBUA DK SHEIN ZANZIBAR


Chama cha Wananchi (CUF) kimesema hakimtambui Dkt. Ali Mohamed Shein aliyetangazwa mshindi wa uchaguzi wa marudio uliofanyika mwezi uliopita.

Wakizungumza kwa mara ya kwanza tangu kufanyika kwa uchaguzi huo wa marudio mnamo Machi 20, mwaka huu, viongozi wa CUF wamesema hawamtambui Dkt Shein kama rais wa visiwa hivyo.

“Tangu mapema pale Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha alipofuta uchaguzi, tulisema waziwazi kwamba halikuwa jambo halali na hata walipoitisha uchaguzi wa marudio tulisema wazi ya kuwa uchaguzi huo hatuutambui na tukawataka wananchi wasipige kura na hatukushiriki,” amesema Katibu Mkuu wa CUF Maalim Seif Sharif Hamad.

Maalim Seif ambaye alikuwa mgombea urais wa chama hicho katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 25, mwaka jana na ambao matokeo yake yalifutwa na tume alihoji kuwa kama Rais ametokana na mchakato ambao hatukuutambua tangu mwanzo, sasa leo kuja kusema hatumtambui kwa nini iwe ni haramu?,na kuongeza kuwa hawamtambui.

Chama hicho kimesema kitatumia njia za kidemokrasia kulalamika dhidi ya Dkt. Shein na serikali yake.

Aidha, kimeiomba jamii ya kimataifa kuwawekea vikwazo watu binafsi waliofanikisha uchaguzi huo wa marudio ambao chama hicho kimesema ulikuwa “uongozi haramu”.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho, Twaha Taslima amesema chama hicho hakiko tayari kuwa sehemu ya serikali mpya.

“CUF haitoshirikiana na serikali itakayoundwa kwa sababu ni kinyume na katiba ya Zanzibar, kinyume na sheria ya uchaguzi na haikutokana na ridhaa ya watu,” amesema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment