Wednesday, 13 April 2016

CALL AFRICA YAJIZATITI KUSAIDIA WATOTO WENYE ULEMAVU IRINGARAIS wa shirika la kimataifa la Call Africa lenye makao yake nchini Italia, Mannini Italo amewataka watanzania kutowanyanyapaa watoto wenye ulemavu wakati kituo chao cha Sambamba kikijipanga kuongeza wigo wa huduma kwa watoto wenye matatizo hayo.

Katika ziara yake aliyoifanya kituoni hapo juzi, Italo alisema baadhi ya watoto wamekuwa wakipata ulemavu kabla na baada ya kuzaliwa kwasababu ya mambo mbalimbali yanayozuilika yakisababishwa na ukosefu wa huduma bora za afya kwa wajawazito.

“Tunataendelea kutoa mchango wetu kwa jamii ya kitanzania, ili watoto hawa wenye ulemavu wapate fursa zitakazoongeza usawa baina yao na wenzao wasio na ulemavu,” alisema.

Alisema wakipata malezi mazuri, wasipobaguliwa, kutengwa na kufichwa, watoto wenye ulemavu watakuwa katika mazingira ya kutoa mchango wao katika jamii kwa kuzingatia uwezo wao.

Alisema nchini Tanzania, Call Africa inayofanya kazi pia katika nchi za Kenya na Zambia katika bara la Afrika ilianzisha huduma kwa watoto wenye ulemavu wa kati ya miaka miwili na 15 katika kituo chake cha Sambamba kwa lengo la kuboresha maisha yao na kupinga unyanyapaa wanaofanyiwa katika jamii.

“Tunatoa pia mafunzo ya ujasiriamali kwa wazazi wa watoto hao na semina ya elimu ya ushiriki na kampeni ya ufahamu kuhusu ulemavu,” Rais huyo alisema. 


Alisema mbali na huduma hizo wanashirikiana na wadau wengine kuwezesha mpango wa chakula mashuleni unaonufaisha wanafunzi 7,000 wa shule mbalimbali za msingi za mjini Iringa.

Alisema katika kipindi cha mwaka huu, kituo cha Sambamba kinatarajia kuongeza huduma zake ili wawafikie watoto wengi zaidi wenye ulemavu katika kata mbili za Ruaha na Kitwiru wanazofanya nazo kazi.

Mwakilishi wa shirika hilo nchini, Umberto Bosco alisema katika kituo hicho watoto hao wanapata huduma mbalimbali ikiwemo ya elimu, michezo, huduma za matibabu, lishe, stadi za maisha na ushauri wa kisaikolojia.

Bosco alisema mpaka sasa kituo hicho kinatoa huduma kwa watoto wenye ulamavu 50 huku lengo lao likiwa ni kuwafikia watoto 150.

“Wakiwa kituoni watoto hao wanafundishwa mambo mbalimbali kutegemea na aina ya ulemavu wao. Na stadi za maisha wanazofundishwa zinalenga kuwawezesha kuwapunguzia utegemezi kwa kadri wanavyokua,” alisema.

Akitoa mfano alisema watoto hao wanafundishwa kuoga, kutumia mswaki kusafisha meno, kuvaa nguo, kusema au kuonesha kwa vitendo kitu au jambo wanalotaka kufanya. 


Alisema kituo hicho kinafanya kazi kati ya Jumatatu na Ijumaa ya kila wiki kwa msaada wa wafanyakazi wajuzi wa huduma kwa watoto, ulemavu na elimu.  

Reactions:

0 comments:

Post a Comment