Monday, 25 April 2016

CAG AANIKA UOZO WA UDA, VYAMA VYA SIASA


Serikali imeshauriwa kulirejesha Shirika la Usafirishaji Dar es Salaam (UDA) katika himaya yake kutoka kwa mwekezaji hadi pale mkanganyiko wa mgongano wa kimaslahi utakapotatuliwa.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali, Prof. Mussa Assad alipokuwa akiwasilisha ripoti ya ukaguzi na kuongeza kuwa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la UDA iliuza hisa za shirika hilo bila ya kupata kibali kutoka Serikalini.

Amesema kwa mujibu wa Mlipaji Mkuu wa Serikali (PST), Serikali haitambui uuuzwaji huo wa hisa, na yeye ndiye mmiliki wa hisa hivyo akisema haitambui maana yake ni kwamba hakuna mauzo yaliyotokea.

“Ni vyema UDA likarudishwa chini ya usimamizi wa serikali kwasababu Serikali haitambui uuzwaji huu wa hisa hadi pale mgogoro huo utakapotatuliwa na tunaamini hatua hizi zinaendelea kuchukuliwa,” ameongeza CAG.

Wakati huohuo CAG, amesema kati ya vyama vya siasa 22 vyenye usajili wa kudumu ni chama kimoja tu cha siasa kilichowasilisha hesabu zao kwa CAG hadi kufikia Juni, 2015. Chama hicho ni Chama cha Wananchi (CUF) kilichowasilisha hesabu zao kwa ajili ya ukaguzi.

“Tunamshauri Msajili wa Vyama vya Siasa aweze kufatilia vyama hivyo vyenye usajili wa kudumu vinawasilisha hesabu zao ili ukaguzi uweze kufanyika kama sheria inavyotaka,” ameongeza Prof. Assad.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment