Monday, 4 April 2016

ASILIMIA 70 YA MAZAO YA MISITU HUPOTEA WAKATI WA UVUNAJI


ASILIMIA 70 ya mazao ya misitu hupotea wakati wa uvunaji kwasababu ya matumizi ya teknolojia iliyopitwa na ujuzi mdogo kwa baadhi ya watendaji wa sekta hiyo jambo linalopunguza mapato kwa wadau wa sekta hiyo na serikali.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, Programu ya Panda Miti Kibiashara (PFP) kwa kushirikiana na Wataalamu wa Mitaala (curricula experts) wameandaa mitaala ya misitu na viwanda vya misitu itakayotumiwa na wadau katika ngazi ya vyuo vya ufundi stadi ili kupata watendaji watakaongeza tija katika sekta hiyo.

Akizungumza katika mkutano uliojadili mitaala hiyo hivikaribuni mjini Iringa, Afisa Mafunzo wa Programu ya Panda Miti, Julius Sonoka alisema wadau wa sekta hiyo wataendelea kupata hasara kubwa kama wataendelea kutumia mashine za kizamani katika uvunaji.
Alisema utafiti unaonesha matumizi ya mashine za kisasa yanasaidia kupunguza upotevu wa mazao ya misitu  kutoka asilimia 70 hadi 30 jambo linaloifanya sekta hiyo iwe na tija zaidi.

Sonoka alisema kukamilika kwa mitaala hiyo kutawawezesha wavunaji na wafanyakazi wengine wa sekta hiyo kupata ujuzi utakaoboresha kazi zao tofauti na ilivyosasa ambapo wengi wao wanafanyakazi kwa kutumia uzoefu.

“Mitaala hii itawawezesha wadau kuongeza ujuzi katika kuihudumia sekta hii kwa kupitia mfumo rasmi ya elimu unaotolewa katika vyuo vya ufundi stadi,” alisema.

Katibu wa Chama cha Wavunaji wenye Viwanda vya Mbao katika Msitu wa Saohill Mufindi (SAFIA), William Mgowole alisema wavunaji wengi wanatumia mashine aina ya digdong na kuingia katika hasara inayozungumzwa kwasababu nyingi ya mashine hizo teknolojia yake ni ya kizamani.

Mgowole alisema ili kupeukana na hasara hiyo wavunaji wanashauri kutumia mashine za kisasa aina ya bed saw zinazosaidia kudhibiti upotevu wa mazao ya misitu chini ya asilimia 30.

 Rais wa Shirikisho la Viwanda vya Misitu Tanzania (Shivimita), Ben Sulusi alisema kuna jumla ya viwanda 300 vya mazao ya misitu nchini na kati yake 70 ni vikubwa ambavyo vinatumia mashine za kisasa na vilivyobaki 230 vinatumia mashine za zamani zinazoruhu upotevu mkubwa.

Akizungumzia umuhimu wa mitaala hiyo alisema itasaidia uzalishaji wa malighafi bora kwani itatoa wataalamu wa miti kuanzia upandaji, uvunaji mpaka kiwandani na kuwa itaondoa matumizi ya wafanyakazi wasiokuwa na ujuzi wowote kwenye sekta hiyo.

Naye Afisa Misitu Mkuu wa Msitu wa Taifa (Sao Hill), Salehe Bereko alisema wadau wa misitu wataweza kupata taaluma sahihi na kuongeza uzalishaji na kutosheleza mahitaji ya soko la ndani na nje.

Alisema kutokana na kupungua kwa mgao wa uchakataji wa mazao ya misitu kutoka meta za ujazo milioni moja mpaka 600,000 kwa mwaka  upandani wa miti kitaalamu na matumizi ya teknolojia ya kisasa inayopunguza upotevu wa mazao wakati wa uchakataji ndio njia sahihi ya kukabiliana na changamoto hiyo.  


Naye Mhandisi Julius Mwakasasa kutoka Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) ambaye ni mkufunzi wa mitambo alisema VETA ipo tayari kushirikiana na wadau kuzalisha watendaji wa sekta hiyo wenye ujuzi watakaofanya kazi zao kwa weledi na viwango chini ya wasimamizi wenye taaluma ya kutosha ya misitu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment