Tuesday, 26 April 2016

Al-Shabab wavamia na kudhibiti kambi ya jeshi Somalia

Wapiganaji wa al-Shabab wamekuwa wakishambulia kambi za jeshi miezi ya karibuni
Wapiganaji wa kundi la al-Shabab walishambulia kambi ya jeshi nchini Somalia na kuidhibiti kwa muda mapema asubuhi kusini magharibi mwa nchi hiyo.
Wapiganaji hao walishambulia kambi ya Jeshi la Taifa la Somalia (SNA) katika eneo la Daynuunay, wilaya ya Baidoa katika jimbo la Bay.
Taarifa zinasema magari zaidi ya kumi ya jeshi la Somalia yaliuawa wakati wa shambulio hilo.
Msafara wa wanajeshi wa Somalia kutoka mji wa Baidoa, waliokuwa wakipelekwa kuwasaidia wenzao, pia ulishambuliwa.
Taarifa zinasema kulitokea vifo na majeruhi pande zote.
Afisa mmoja wa serikali eneo hilo ameambia BBC kwamba watu zaidi ya 10 walifariki.
Mwandishi mmoja wa eneo hilo ameambia BBC kwamba wanajeshi 20 waliuawa wakati wa shambulio hilo.
Kikosi cha Umoja wa Afrika (Amisom) kimesema kupitia Twitter kwamba shambulio hilo lilitokea lakini kikakanusha taarifa kwamba kambi hiyo ilidhibitiwa na wapiganaji hao.
Kambi hiyo inapatikana kilomita 30 kutoka mji wa Baidoa.
Al-Shabab wamezidisha mashambulio dhidi ya wanajeshi wa Amisom na Somalia tangu katikati mwa mwaka jana.
Mapema mwaka huu, walishambulia kambi ya wanajeshi wa Kenya wanaohudumu chini ya Amisom.
Al-Shabab wamesema kwamba waliua zaidi ya wanajeshi 200 katika shambulio hilo eneo la El-Ade katika jimbo la Gedo tarehe 15 Januari mwaka huu.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment