Monday, 14 March 2016

TAKUKURU YAANZA KUCHUNGUZA TAARIFA ZA LUKUVI KUHUSU MLUNGULA WA BILIONI 5

Image result for lukuvi

Taaasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) imesema kuwa inaanza kuchunguza taarifa zilizotolewa hivi karibuni na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kuwa alishawishiwa kupokea rushwa ya shilingi bilioni 5 na wafanyabiashara wawili wakubwa.

Mkurugenzi wa TAKUKURU, Valentino Mlowola amesema kuwa taasisi hiyo imeshaanza kufanyia uchunguzi taarifa hizo ikiwa ni mpango wake mpya wa kuchunguza kila taarifa ya rushwa inatolewa.

“Kufafanua kuwa tumeanza lini hilo ni suala la kiufundi, ila la msingi ni kuwa tumeshaanza kulishughulikia,” ameongeza Mlowola.

Hivi karibuni Waziri Lukuvi alinukuliwa akisema kuwa alikataa kiasi hicho cha fedha alichoahidiwa na wafanyabiashara wawili wakubwa waliotaka awasaidie kupitisha mpango wao wa kuiuzia Serikali ardhi ya mabilioni ya fedha katika eneo lililopangwa kujengwa mji mpya wa Kigamboni.

Waziri Lukuvi alizidi kufafanua kuwa wafanyabiashara hao walinunua ardhi kutoka kwa wananchi kwa gharama ya shilingi milioni 5 kwa ekari moja na kutaka kuiuzia Serikali ardhi hiyo kwa shilingi milioni 141 kwa ekari moja tu.

“Niligundua pale kuna udanganyifu na wizi mkubwa. Haiwezekani mwekezaji anunue ardhi kutoka kwa wananchi kwa shilingi milioni 5 tu alafu aitake Serikali ilipe shilingi milioni 141 kwa ekari hiyohiyo  moja kwa kuvuka pantone tu. Huu ni wizi mkubwa,” alinukuliwa Waziri Lukuvi.

Alisema wafanyabiashara hao waliwaeleza marafiki zake wa karibu ya kuwa wamepanga kumpa kiasi hicho cha fedha kama rushwa ili kuupitisha mpango wao lakini ilishindikana kwake.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment