Sunday, 13 March 2016

SHULE YA WALEMAVU MAKALALA MAFINGA YAWAPIGIA MAGOTI WASAMARIA WEMA
SHULE ya Msingi ya Walemavu ya Makalala iliyopo mjini Mafinga mkoani Iringa inazidi kuelemewa na changamoto zinazohitaji serikali na wadau wake kuinusuru ili kuwatenda haki wanafunzi wanaosoma na wanaohitaji kujiunga nayo.

Shule hiyo yenye wanafunzi 79, ina mwalimu mmoja tu wakati mahitaji ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano.

Akizungumza na wanahabari waliotembelea shule hiyo juzi, Mkuu wa shule hiyo, Shem Muheni alisema haina mabweni ya kutosha jambo lililosababisha ishindwe kupokea wanafunzi wengi waliotaka kujiunga mwaka huu.

“Wanafunzi wengi wako nyumbani, tunashindwa kuwapokea kwasababu ya uhaba wa mabweni, hapa tuna mabweni mawili tu kwa wanafunzi wa kike na kiume ambayo hayakidhi mahitaji ya wanafunzi waliopo,” alisema.

Alisema miundombinu ya mabweni hayo ni ya zamani kwani mbali na kutokuwa rafiki kwa wanafunzi hao wakati wakitoka na kuingia ndani, madirisha yake hayafunguki na yana vitanda vichache ambavyo havikidhi mahitaji.

Wakati shule hiyo ikiwa katika wilaya inayoongoza kwa kuwa na misitu ya kupandwa nchini(msitu wa Taifa wa Saohill), Muheni alisema wanafunzi hao wanalala wawili badala ya mmoja kwa kila kitanda huku bwalo la chakula likiwa na meza nne tu wakati mahitaji ni zaidi ya meza kumi.

“Lakini pia hawana nguo, viatu na vifaa vya kujifunzia ambavyo havitoshelezi mahitaji yao ya kila siku,” alisema.

Kuhusu chakula, Muheni alisema pamoja na kwamba serikali imekuwa ikitekeleza wajibu wake wa kupeleka chakula shuleni hapo hasa unga na maharege, wanafunzi hao wanahitaji kula vyakula mchanganyiko ili kukidhi mahitaji yao ya mwili na akili.

Mbunge wa jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi alitoa wito kwa watu mbalimbali kuguswa na matatizo ya wanafunzi na shule hiyo kwa kuchangia kile walichonacho ili changamoto zilizopo zipungue au zimalizike kabisa.

Kuhusu uhaba wa walimu na mabweni, Chumi alisema serikali inatakiwa kuitazama shule hiyo kwa jicho la huruma ili mahitaji hayo yapatikane.

“Shule inahitaji mabweni ya ziada na yaliyopo yakarabatiwe; wito wangu kazi hii isiachwe kwa serikali pekee yake, tunaomba wadau wetu wajitokeze kusaidia kuboresha miundombinu hiyo na kushughulikia changamoto zingine,” alisema.

Shule hiyo inayochukua wanafunzi wasioona na wenye ulemavu wa akili kutoka maeneo mbalimbali nchini ilianzishwa mwaka 1954.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment