Sunday, 13 March 2016

SERIKALI YAWATOLEA UVIVU WAATHIRIKA WA MAFURIKO WALIORUDI KATIKA ENEO LA HIFADHIWIKI tatu baada ya mtandao huu kuripoti taarifa ya baadhi ya waathirika wa mafuriko katika eneo Tengefu la Nyaruu kata ya Pawaga wilayani Iringa mkoani Iringa kurejea kinyemela katika eneo hilo baada ya kuokolewa, Kamati za Ulinzi Mkoa na Wilaya ya Iringa zimetoa tamko zito linalowataka waondoke mara moja.

Mbali na kulima katika eneo hilo ambalo ni makutano ya mto Ruaha Mdogo na Mto Ruaha Mkuu, na ambalo pia ni la mapito ya wanyamapori wanaotoka katika hifadhi za Taifa za Ruaha na Mikumi; linadaiwa ni maficho ya majangili wa wanyamapori kwasababu ya kuwepo kwa shughuli za kibinadamu.

Waathirika hao wadaiwa kuanza kurejea katika aneo hilo baada ya maji kuanza kupungua wakilindwa na kauli zilizokuwa zikitolewa na baadhi ya viongozi waliokuwa wakiwataka waendelee kulitumia eneo hilo kwa shughuli za kilimo bila kujua kwamba eneo hilo limehifadhiwa kwa mujibu wa sheria inayounda jumuiya za wanyamapori.

“Naagiza hakuna kurudi tena Nyaruu, Nyaruu ni eneo tengufu lililohifadhiwa na litaendelea kubaki tengufu, sitaki kugombana na mtu yoyote, najua mlikuwa mnalitumia eneo hilo kujipatia mapato, nawaambia ni marufuku kwa kuwa mlikuwa mkifanya hivyo kinyume cha sheria,” Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Mkoa wa Iringa alisema.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi ya Wilaya ya Iringa ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela alisema; “tangazo likishatoka kinachobaki ni utekelezaji tu, eneo tumeshalirudisha kwenye hifadhi, niwatangazie rasmi yoyote atakayerudi kule atakamatwa na kushughulikiwa.”

Akizungumza na gazeti hili hivikaribuni, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wanyamapori Tarafa ya Pawaga na Idodi (Mbomipa) inayohifadhi eneo hilo, Christopher Mademla alisema watu hao wanaoendesha kinyemela shughuli zao za kilimo na ujangili katika eneo hilo la hifadhi walianza kurejea siku chache baada ya kuokolewa.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment