Tuesday, 1 March 2016

SERIKALI YATAKA BALOZI SEFUE ASAFISHWE


Serikali imelitaka gazeti la Dira ya Mtanzania kumuomba radhi Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue kufuatia habari iliyoiandika yenye kichwa cha habari ‘Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu’.

Gazeti hilo la February 29, lilimtuhumu Sefue kushawishi juu ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Kampuni za ‘CRJE’ na ‘UGG’ kupewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na Reli ya Dar es Salaam – Kigali.

Taarifa ya serikali kwa vyombo vya habari imesema Sefue hakuhusika kwa namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD na kwamba alichofanya Sefue ni kutangaza uteuzi wa raisi na sio vinginevyo.

Kuhusu kampuni ya CRJE, serikali imesema jambo hilo ni la uzushi kwani kampuni hiyo ilipewa tenda ya ujenzi wa chuo mwaka 2007 muda ambao Sefue alikuwa Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York.

Vilevile serikali imesema balozi Sefue hajawahi kuipigia chapuo kampuni yenye jina la UGG na kwamba hakuna kampuni yenye jina la ‘UGG’ iliyowahi kuonesha nia ya kujenga reli ya kati.

“Kwa sababu hiyo, Serikali inalitaka Gazeti  la  Dira ya Mtanzania  kukanusha uongo na uzushi wao na kumuomba radhi Balozi Ombeni Sefue, kuiomba radhi Serikali na kuwaomba radhi wote walioumizwa na uzushi huo kwa uzito ule ule uliotumika kuchapisha taarifa hiyo,” taarifa hiyo ilisema.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment