Tuesday, 1 March 2016

NAIBU WAZIRI TAMISEMI AMTOLEA UVIVU MENEJA WA MAMLAKA YA MAJI KISARAWE


Naibu Waziri Ofisi ya Rais TAMISEMI, Utumishi na Utawala bora, Jafo Selemani Said amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe kumtafutia kazi nyingine Meneja wa Mamlaka ya Bodi ya Maji Kisarawe, Listern Materu kutokana na kushindwa kutatua kero ya maji kwa muda mrefu.

Jafo ambae pia ni mbunge wa jimbo la Kisarawe amesema hawawezi kuendelea kukaa na watumishi ambao hawaguswi na matatizo ya wananchi.

Naibu Waziri huyo alimtaka Materu kuachia nafasi ya Meneja ili apangiwe kazi nyingine kwani ameshindwa kutatua changamoto ya maji katika mji wa Kisarawe.

“Mkurugenzi mtafutie kazi nyingine katika ofisi yako, hatuwezi kuwa na watu ambao hawaguswi na matatizo ya watu tafuta atakayekaimu nafasi yake katika kipindi hiki kwasababu hatufanyi mambo ya kuchekeana na  kamwe hatuwezi kuibadilisha Kisarawe yetu kama tutaendelea kuwavumilia watumishi wanaochangia kudumaza maendeleo”alisema Jafo.

Inadaiwa kuwa Materu amekuwa Meneja wa Mamlaka hiyo kwa zaidi ya miaka kumi lakini hakuna njia mbadala iliyobuniwa na mamlaka hiyo kuondoa tatizo la maji kukosekana mara kwa mara.

Mji huo wa Kisarawe una chanzo cha maji cha Kimani ambacho kinatoa lita 16,000 kwa saa na chanzo kingine cha Minaki kinachotoa zaid ya lita 10,000 kwa saa hali ambayo ni dhahiri kusingekuwepo na tatizo la maji.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment