Tuesday, 15 March 2016

NAIBU WAZIRI ATOA MAAGIZO YATAKAYOPUNGUZA MATATIZO YA SHULE YA WALEMAVU MAFINGA

NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Tamisemi, Utumishi na Utawala Bora, Selemani Jaffo ametoa maagizo matatu yatakayowanusuru wanafunzi walemavu wanaosoma katika shule ya msingi ya Makalala Mchanganyiko iliyopo mjini Mafinga, wilayani Mufindi mkoani Iringa.

Jaffo ametoa maagizo hayo baada ya juzi kufanya ziara ya ghafla shuleni hapo ikiwa ni siku kadhaa toka baadhi ya vyombo mbalimbali vya habari viripoti changamoto zinazowakabiri wakabili wanafunzi na shule hiyo.

Changamoto hizo ni pamoja na udogo na uchakavu wa mabweni ya wanafunzi, uhaba wa walimu na watumishi wengine wa shule hiyo; na ukosefu wa vifaa vya kufundishia na michezo pamoja na mahitaji mengine mbalimbali muhimu kwa wanafunzi na wafanyakazi wa shule hiyo.

Akiwa shuleni hapo, Jaffo alibaini shule hiyo kugubikwa na matatizo hayo kwasababu watendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mufindi ambayo awali shule hiyo ilikuwa chini yake na sasa halmashauri ya Mafinga Mji kwa pamoja wamekuwa hawaifuatilii kwa jicho la jirani pamoja na kwamba ina mahitaji maalumu.

Waziri huyo alisikitishwa matroni pekee wa wanafunzi hao wenye ulemavu Faraja Mbilinyi aliposema kwa miaka 15 halmashauri ya wilaya ya Mufindi haijawahi kumlipa malipo yake ya likizo, huku Mwalimu Agne Jalu mwenye ulemavu wa macho akisema hajawahi kupata malipo kamili ya likizo tangu aanze kulipwa.

Akitoa agizo la kwanza baada ya kutembelea mabweni ya shule hiyo na kusikia kilio cha matroni na mwalimu huyo, Jaffo alisema; “hakikisheni walimu na watumishi wa shule hii ya walemavu na shule yake dada kama wanadai posho malimbikizo ya posho zao likizo wanalipwa mara moja na wanapandishwa madaraja haraka iwezekanavyo.”

Akimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jowika Kasunga kusimamia maagizo aliyokuwa akiyatoa waziri huyo alisema April 1 atapita kwa mara nyingine shuleni hapo ili kujionea utekelezaji wa maagizo yake ambayo yaliahidiwa na Mkurugenzi wa Mafinga Mji, Shaibu Nnunduma kutekelezwa.

Kuhusu ufinyu wa mabweni na uchakavu wake, naibu waziri Jaffo alitoa agizo la pili kwa halmashauri ya mji huo ianze ujennzi wa bweni lingine kwa kutumia vyanzo vyake  vya mapato huku akitaka mpaka mwishoni mwa mwezi April, magodoro yote katika bweni la wasichana na wavulana wa shule hiyo yawe yamebadilishwa.

“Mji wa Mafinga ni mji wa biashara, waiteni wadau wenu, waelezeni matatizo ya shule hii, nina hakika mtachangiwa. Msissubiri kila kitu kifanywe na serikali kuu, hiyo haitawezekana,” alisema.

Kuhusu vifaa vya kufundishia na kujifunzia, alitoa agizo la tatu akiitaka halmashauri hiyo kuhakikisha shule hiyo inakuwa na vifaa hivyo kulingana na mahitaji yake.

Alisema inashangaza kuona watendaji na wadau wao wengine kila wanapokutana katika vikao vyao wanalipana posho halafu wakashindwa kupata fedha kwa ajili ya kushughulikia matatizo ya shule hiyo maalumu.

Awali Mkuu wa shule hiyo mchanganyiko, Shem Muheni alisema shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1954 ina wanafunzi 544 ambao kati ya 79 ni wanafunzi wenye ulemavu wa akili, ngozi na macho wanaosoma katika shule maalumu shuleni hapo.

Alisema wakati mahitaji ya walimu katika shule hiyo ya walemavu ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi watano, ina mwalimu mmoja na matroni mmoja aneyalazimika kuwahudumia kwa pamoja wanafunzi wa kike na kiume.

Alisema uhaba wa vyumba vya kusomea na mabweni umeifanya shule hiyo ishindwe kupokea idadi kubwa zaidi ya wanafunzi wanaotaka kujiunga nayo.

Ikiwa katika wilaya inayoongoza kwa kuwa na misitu ya kupandwa nchini(msitu wa Taifa wa Saohill), Muheni alisema wanafunzi hao walemavu wanalala wawili badala ya mmoja kwa kila kitanda huku bwalo la chakula likiwa na meza nne tu wakati mahitaji ni zaidi ya meza kumi.

“Lakini pia hawana nguo, viatu na vifaa vya kujifunzia ambavyo havitoshelezi mahitaji yao ya kila siku,” alisema.


Hivi karibuni Mbunge wa Jimbo la Mafinga Mjini, Cosato Chumi alitoa wito kwa wadau wa maendeleo wa wilaya ya Mufindi kujitokeza kusaidia kuzishughulikia changamoto za shule hiyo.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment