Friday, 11 March 2016

MALI ZA KINARA WA DAWA ZA KULEVYA KUTAIFISHWA

Mfanyabiashara wa dawa zilizopigwa marufuku za kulevya kutoka Tanzania, Ali Khatib Haji Hassan.

Mali za mfanyabiashara wa dawa za kulevya kutoka Tanzania, Ali Khatib Haji Hassan, maarufu kwa jina la “Shikuba zimetaifishwa na serikali ya Marekani.

Shikuba,  anadaiwa kujihusishwa na biashara kubwa ya usafirishaji dawa za kulevya kati ya Afrika Mashariki, Asia, Ulaya na Marekani, alikamatwa mwaka 2014 nchini Tanzania akihusishwa na shehena ya kilo 210 za heroin zilizokamatwa mkoani Lindi mwaka 2012.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa juzi na kitengo cha udhibiti wa mali za nje cha Wizara ya Fedha ya Marekani imeeleza kuwa serikali imemtambua Shikuba kama kinara wa usafirishaji wa dawa za kulevya kwa mujibu wa Sheria ya Utambuzi wa Vinara wa Dawa za Kulevya wa Nje (Foreign Narcotics Kingpin Designation Act) ya Marekani.

“Hassan  ni kinara mkubwa wa kimataifa wa dawa za kulevya ambaye anasafirisha mamilioni ya tani za heroine na cocaine kwenda barani Afrika, Asia, Amerika Kaskazini kwa kutumia mtandao wake uliopo Afrika Mashariki,” inasema taarifa hiyo ya Serikali ya Marekani iliyotolewa Washington juzi.

“Kutokana na uamuzi wa leo (juzi), mali zote za Hassan na mtandao wake ambazo ziko ndani ya mamlaka ya Marekani au kwenye mikono ya raia wa Marekani zinataifishwa.”

Marekani ilipitishwa Sheria hiyo  mwaka 1999 na kuanza kazi mwaka uliofuatia, ikiwa na lengo la kudhibiti wasafishaji wa dawa za kulevya, biashara na shughuli zao kuingia kwenye mfumo wa kifedha wa nchi hiyo na kudhibiti biashara na miamana baina ya wasafirishaji wa dawa hizo na kampuni za Marekani na raia wake.

Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, sheria hiyo imekuwa ikitumiwa na Marekani kufuatilia wahalifu kadhaa wanaojihusisha na biashara hiyo duniani.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya Marekani, Hassan amekuwa akijaribu mara kadhaa kurubuni viongozi wa Serikali za Afrika kuepuka kukamatwa na kufunguliwa mashtaka kutokana na biashara zake haramu.

 “Wasafirishaji wa dawa za kulevya kama Mtandao wa Usafirishaji Dawa za Kulevya wa Hassan ni tishio kubwa kwa uthabiti wa mfumo wa kimataifa wa fedha na kanda, na Hazina inaendelea kuwa thabiti katika kuuanika na kufuatilia na wale wanaochochea biashara hiyo duniani.”

Tangu mwaka 2006, amekuwa akiongoza wanachama wa mtandao wake kutuma shehena za dawa hizo kwenda sehemu kadhaa duniani kama China, Ulaya na Marekani.

Hassan alikuwa msambazaji wa kwanza kwa wasafirishaji dawa za kulevya wa Tanzania ambao mara kwa mara walikuwa wakipokea maelfu ya kilo za heroine kutoka pwani ya Makran nchini Pakistan na Iran.


Reactions:

0 comments:

Post a Comment