Tuesday, 22 March 2016

KITWIRU, ISAKALILO, NGELEWALA NA MAWELEWELE KUNUFAIKA NA MRADI WA MAJISAFI KITWIRU


MKUU wa Mkoa wa Iringa, Amina Masenza leo amezindua ujenzi unaondelea wa mradi wa majisafi Kitwiru unaolenga kuboresha huduma ya majisafi kwa kaya 900 za manispaa ya Iringa, wakati wa kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji mkoa wa Iringa.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Iringa Mjini (IRUWASA), Gilbert Kayange alisema mradi huo ulioanza kujengwa Julai mwaka jana, unatarajia kukamilika Julai mwaka huu.

Kayange alisema utakapokamilika, mradi huo utaongeza uzalishaji wa maji toka mita za ujazo 218 hadi 1,200 kwa siku na kuzinufaisha kaya hizo zilizopo katika maeneo ya Kitwiru, Ngelewala, Mawelewele na Isakalilo.

Alisema mradi huo unajengwa kwa zaidi ya Sh Milioni 700 ambazo kati yake Sh Milioni 550 ni za mkopo toka CRDB benki na Sh Milioni 150 za makusanyo yao ya ndani.

“Mradi unahusisha ujenzi wa nyumba ya mitambo, bomba la usambazaji majisafi, tanki la maji la mita za ujazo 340, mitambo ya kusukuma maji na utanuzi wa mtandao wa usambazaji maji safi wenye urefu wa kilomita 10,” alisema.

Akizitaja faida za mradi huo pindi utakapokamilika, Kayange alisema utaongeza upatikanji wa huduma ya maji safi kwa saa 24 kwa siku, utapunguza gharama ya maunganisho mapya kutokana na miundombinu ya majisafi kupita karibu na makazi ya wananchi na utaondoa tatizo la magonjwa yanayosababishwa na uhaba wa maji yasio safi na salama.

Ili utoe huduma endelevu, alisema kutakuwa na ukarabati na matengenezo ya miundombinu yake kwa wakati, watahamasiaha kulinda miundombinu hiyo, mazingira na uhifadhi wa vyanzo vya maji.

Akitoa taarifa ya mkoa katika madhimisho hayo, Mkuu wa Mkoa alisema asilimia 71.2 ya wakazi wa mkoa wa Iringa huduma ya maji safi na salama.

Masenza alisema utunzaji wa mazingira ni jambo muhimu kwa uendelevu wa rasilimali ambayo ni muhimu kwa maisha na maendeleo ya binadamu zikiwemo shughuli za kiuchumi.

Katika upatikanaji wa maji mijini na vijijini, alisema ipo haja ya kutumia teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua hasa katika maeneo yenye upungufu wa huduma hiyo.

“Lakini pia tuangalie jinsi ya kutmia teknolojia ya kutumia nguvu ya jua na nguvu ya upepo katika kusukuma maji, teknolojia hizi ni rahisi hasa kwenye ngazi ya kaya na ngazi ya taasisi,” alisema.

Reactions:

0 comments:

Post a Comment